Header Ads

DC AKERWA NA UHUJUMU WA MSITU.









PEMBA.
Wananchi wa shehia ambazo zimezunguka msitu wa hifadhi wa ngezi vumawimbi wakishirikiana na idara ya mazingiza kisiwani Pemba wametakiwa kuuona msitu huo kama ni wa kwao kwa kuongeza uhifadhi wa kukabiliana na vitendo uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya watu ndani yam situ huo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Micheweni  Abeid Juma Ali kwenye kikao kilicho wakutanisha baadhi ya watendaji wa idara ya misitu, Jeshi la polisi, masheha pamoja na wazee ambao wanaishi katika shehia ambazo zimezunguka msitu huo, kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa wilaya.

Alisema kumekuwepo na vitendo vya uhalifu kwa baadhi ya watu kuvamia msitu huo na kufanya uhalifu kwa kukata miti ovyo jambo ambalo likifumbiwa macho litapelekea kutoweka  kwa hifadhi hiyo.

“ suala la uvamizi wa misitu ni suala baya ambalo kama halikuchukuliwa hatua linaweza kuleta athari mbaya zaidi hapo baadae, mimi kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya micheweni sitofumbia macho vitendo kama hivi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakao bainika” alisema DC.

Kwa upande wake Afisa uhusiano wa viumbe na miti kisiwani Pemba Salim Mohammed Said alikiri kuwepo kwa uhujumu huo wa kukatwa miti ndani msitu huo jambo ambalo linafanywa na baadhi ya watu.

Alisema msitu wa ngezi wenye ukubwa wa hekta 2900 ni hazina kubwa sana hapa Zanzibar ambapo mwaka 1959 ulitangazwa rasmi kuwa sehemu ya hifadhi, licha ya baadhi ya watu kufanya uhujumu ndani yam situ huo.

Alizitaja changamoto ambazo zinaikabili hifadhi hiyo alisema ni pamoja na wizi wa miti mikuwa ya mbao, wizi wa miti ya kujengea, upikaji wa pombe haramu aina ya gongo unaopelekea moto na uharibifu mwengine wa kimazingira katika msitu huo, uvamizi wa mipaka ya msitu kwa shuhuli ya kilimo pamoja na uchungaji wa mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi. 

Alizitaja sababu zinazopelekea kuwepo kwa changamoto hizo ni pamoja uhaba wa walinzi wa msitu huo ambapo msitu wenye ukubwa wa hekta 2900 una walinzi nane, mashirikiano madogo kati ya jamii inayozunguka msitu na walinzi wa msitu, mashirikiano madogo kati ya uongozi wa shehia na walinzi wa msitu, kucheweshwa kwa kutolewa maamuzi kwa kesi za uharibifu ambazo zinaripotiwa vituo vya polisi pamoja na kutolewa kwa adhabu ambazo haziendani na sharia za misitu.

“ walinzi nane wa serikali kwa msitu wenye ukubwa wa hekta 2900 ni kidogo sana na ndo mana wahalifu wanapata fursa ya kufanya uhujumu katika msitu huo, ili kuepusha uhalifu usiendelee lazima walinzi waongezwe, mashirikiano yawepo kwa walinzi na watu wa karibu ” alisema Salim.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa kituo cha Polisi Konde  Koplo Hamad Omar Khamis alisema jeshi la Polisi linatoa mashirikiano  makubwa kwa idara ya misitu katika suala zima la kupambana na watu wanaohusika na matendo ya uhujumu wa msitu huo.
Alikanusha baadhi ya maneno ambayo yanazungumzwa na baadhi ya wananchi ya kuwa jeshi la polisi kituo cha Konde linashirikiana na wahalifu hao, alisema hilo sio la kweli na zipo kesi nyingi zinazo husiana na masuala hayo ambazo zinaendelea kufatiliwa na nyengine zipo mahakamani.

“ si kweli kuwa jeshi la polisi kituo cha konde linashirikiana na wahalifu hao, mimi binafsi nashirikiana vilivyo na idara ya misitu na nimeshawahi kuenda katika ukamataji wa wahalifu hao na hadi sasa yupo mtuhumiwa ambae kila baada ya siku mbili anakuja kuripoti kituoni” alisema Koplo Hamad.

Sheha wa shehia ya makangale Mohammed Juma Ali alisema eneno la sijuu ambalo liko katika shehia ya makangale ni moja mwa eneo ambalo linatumika sana na wahalifu wanaofanya uhalifu ndani ya msitu huo.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake Mkubwa Said Ali mkaazi wa shehia ya Tondooni  alisema ipo haja ya kuongezwa kwa walinzi wa msitu huo na itakua kitu cha busara sana endapo walinzi hao watatokea katika vijiji ambavyo vinauzunguka msitu huo.

No comments