DR SHEIN AWATAKA VIONGOZI PAMOJA NA WANANCHI KUUNGA MKONO KAMISHENI YA KISWAHILI.
Zanzibar
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi pamoja na wananchi wake
wataendelea kuiunga mkono Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa lengo la kuiimarisha lugha ya Kiswahili ambayo inaendelea kujipatia
umaarufu mkubwa duniani kote.
Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na
mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki Profesa Kenneth Linyani Simala, Ikulu Mjini Zanzibar.
Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa
kuna kila sababu ya kuendelea kuiunga mkono Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki ambayo kwa hivi sasa Makao makuu yake yapo hapa Zanzibar
kwa kutambua kuwa asili na chimbuko la lugha ya Kiswahili ni Zanzibar.
Alieleza kuwa Zanzibar imefarajika kwa kiasi
kikubwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uwamuzi wa makusudi wa kuyaweka
makao makuu ya Kamisheni hiyo hapa Zanzibar kwani Zanzibar inahistoria kubwa ya
lugha ya Kiswahili.
Alisisitiza kuwa Afika Mashariki ndio wenye
Kiswahili hivyo ni jambo la busara kuwepo kwa
Kamisheni hiyo ambayo itaendeleza na kukikuza Kiswahili ili kizidi
kuimarika.
Dk. Shein alisema kuwa Kiswahili ni lugha tajiri
na maarufu sana ulimwenguni hivyo kuna haja ya kuchukua juhudi za makusudi
katika kuhakikisha lugha hiyo inazidi kuimarika na kupata mafanikio makubwa
zaidi.
Aidha, Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa
ya uongozi wa Katibu Mtendaji huyo Profesa Simala katika kuiendeleza na
kuiongoza Kamisheni hiyo muhimu kwa nchi za Afrika ya Mashariki.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza haja ya
kukiimarisha zaidi Kiswahili pamoja na kukipa hadhi yake katika kukizungumza
hasa katika mikutano ikiwemo ya Jumuiya hiyo na mengineyo huku akieleza kusikitishwa
kwake na baadhi ya mikutano inayowashirikisha wahusika wengi waswahili hapa
nchini lakini huendeshwa kwa lugha ya kiengereza kwa kisingizo cha udhamini wa
mikutano hiyo.
Dk. Shein alieleza kuwa hali hiyo ni kinyume na
nchi nyengine duniani ambazo zinakuza, zinathamini na kuimarisha lugha zao
ambazo huzipa kipaumbele kwa kutambua umuhimu wake katika kuzipa hadhi lugha
zao.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alieleza haja ya
kukizungumza Kiswahili ili kizidi kuimarika na kukijengea heshima na hadhi yake
kama ilivyo kwa baadhi ya nchi nyengine duniani ambazo hutumia lugha zao kama
lugha za taifa ambapo hutumia hata kusomeshea katika vyuo vyao vikiwemo vyuo
vikuu.
Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki Profesa Kenneth
Linyani Simala alitoa shukurani za dhati
kwa Dk. Shein kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali yake anayoiongoza
kwa kuipokea Kamisheni hiyo pamoja na kuipa jengo ambalo kwa sasa ndio makao
makuu ya Kamisheni hiyo.
Kutokana na juhudi hizo za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, pamoja na zile za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa mafanikio makubwa yatapatikana katika
kukiimarisha Kiswahili kutokana na mashirikiano hayo.
Aidha, Profesa Simala alimueleza Dk. Shein kuwa
Kamisheni hiyo imeweza kukutana na wadau mbali mbali na kuunda mpango mkakati ambao utazinduliwa katika Kongamano la Kiswahili la kwanza
linalotarajiwa kufanyika hapa Zanzibar.
Aliongeza kuwa Kongamano hilo linatarajiwa
kuwashirikisha wajumbe 150 kutoka nchi wanachama zote za Jumuiya ya Afrika
Mashariki pamoja na wajumbe kutoka Uturuki, Burundi, DRC Congo, Burundi,
Rwanda, Namibia, Wanahabari, wanasiasa na washiriki wadau wengine kutoka nchi
mbali mbali duniani.
Alieleza kuwa miongoni wma mambo ambayo wajumbe
hao watajifunza ni pamoja na kuijua historia ya Zanzibar na baadae ripoti
itatolewa kwa viongozi wa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mshariki.
Profesa Simala alitumia futsa hiyo kumueleza Rais
Dk. Sheinazma ya Kongamano hilo la kwanza la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo
linatarajiwa kufanyika hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza kuanzia tarehe 6 hadi
tarehe 8 mwezi ujao.
Sambamba na hayo, Profesa Simala alimueleza Dk.
Shein miongoni mwa majukumu ya Kamisheni hiyo kuwa ni kuwaweka pamoja wadau wa
lugha hiyo ya Kiswahili huku akieleza kuwa tayari kwa upande wa nchi za nje ya
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zimeshatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili
ikilinganshwa na nchi husika za Jumuiya hiyo.
Post a Comment