MKOA KWA KUSHIRIKIANA NA WIZARA YA KILIMO, MIFUGO, NA UVUVI WAPONGEZWA KWA KUYABAINISHA NA KUYAREJESHA SERIKALINI MASHA,MBA YA SERIKALI.
Zanzibar
UONGOZI wa Mkoa wa Kusini Pemba
kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi umepongezwa kwa
kuyabainisha na kuyarejesha Serikalini mashamba ya Serikali na kuagizwa kwa
wale wote ambao bado wanayaficha mashamba hayo ni bora wayarejeshe wenyewe
vyenginevyo wakibainika wawachukulie hatua kali za kisheria.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein aliongeza kuwa hatua hizo kali za
kisheria zichukuliwe bila ya kujali wadhifa wa mtu, cheo alichonacho ama
umaarufu wake.
Agizo hilo limetolewa leo na Dk. Shein huko katika ukumbi wa Makonyo, Jimbo
la Wawi, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba wakati akitoa majumuisho ya
ziara yake kwa Mkoa huo aliyoifanya kuanzia Agosti 24 mwaka huu.
Aidha, Dk. Shein aliuagiza uongozi wa Mkoa huo pamoja na Wilaya zake
kusimamia vizuri ukusanyaji mapato na kushirikiana na wafanyabiashara katika
kuwashajiisha ili walipe kodi na kuongeza mapato ya Serikali.
Aliwataka viongozi hao kutojiingiza katika kuwasaidia kukwepa kodi wala
kuwakingia kifua kwa makosa yao wanayoyafanya katika kukwepa kulipa kodi huku
akiwataka kuwashajiisha wafanyabiashara watoe risiti wanapouza bidhaa zao na
kuwaelimisha wananchi wapewe risiti wanaponunua bidhaa.
Pia, Dk. Shein ameiagiza Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo
kufanya mkutano maalum na Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote za Unguja na Pemba kwa
ajili ya kupanga na kupeana majukumu ya utekelezaji wa mpango wa Utalii kwa
Wote huku akiuagiza uongozi wa Mkoa kushirikiana na Wizara hiyo kulishughulikia
eneo la historia la Mkamandume.
Kwa upande wa wajibu wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. Shein ambaye pia, ni
Makamo Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar aliwataka wanaCCM
kuendeleza umoja na mshikamano uliopo na kuepuka mivutano miongoni mwao na kama
ipo waachane nayo kwani haina tija.
Aliwataka wanaCCM kuandaa utaratibu mzuri wa kusimamia utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM ya mwaka 2015-2020 sambamba na kuyatumia Matawi
ya CCM kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu
ujao.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliuagiza uongozi wa Mkoa na Wilaya zake zote
mbili kushirikiana na Maafisa Ukaguzi wa Elimu katika maskuli na iwapo
watawabaini walimu watoro kazini na wale wanaofanya siasa skuli wamuarifu
Waziri wa Eloimu na Mafunzo ya Amali ili awachukulie hatua kwa mjibu wa sheria
ya Utumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2011.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa majengo ya skuli yanakuwa na ubora
unaotakiwa na kuweza kutumika kwa muda mrefu alitaka Wizara hiyo ya Elimu
kuhakikisha majengo ya madarasa yanayojengwa yanakuwa na mazingira bora na
yenye viwango.
Pia, alitoa agizo kwa uongozi wa Mkoa kuwa soko jipya linalojengwa
katika eneo la Tibirinzi kuanzia jana (25.8.2017) liitwe soko la Tibirinzi
badala ya soko la Katar na kuutaka uongozi huo kulisimamia suala hilo kwa nguvu
zake zote bila ya kugombana na watu.
Dk. Shein alitoa wito kwa Mabaraza ya Miji ya Mkoa huo, kusimamia
vizuri usafi wa Miji pamoja na mipango miji na kutaka kuendelea kuwachukulia
hatua waatu wanaojenga karibu sana na barabara.
Alisisitiza kuwa Mkoa ni lazima uwe na mpango wa muda mrefu wa
kulishughulikia tatizo la nafasi ya maegesho ya gari linaloendelea kujitokeza
katika mji wa Chake Chake.
Aliwataka viongozi wote wa Mkoa
huo kwenda kubainisha halafu watafute mbinu ya kuiondosha hali ya wizi wa
karafuu na ni vyema wakalifuatilia suala hilo ili kuujua ukweli huku akiahidi
kuwa Serikali inatekeleza ahadi yake ya kumpa mkulima asilimi 80 ya bei ya
soko.
Kwa kukinga ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara kisiwani
Pemba pia, Dk. Shein alieleza kupata taarifa ya kuwepo vijana katika eneo la
Chake Chake wenye kuiga nyendo za kundi la ‘T-One hasa nyakati za usiku na
kuutaka Mkoa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wasiozingatia
sheria za barabarani.
Dk. Shein. Alieleza kufurahishwa kwake na upatikanaji wa maji katika
Mkoa wa Kusini Pemba ambao umefikia asilimia 83.
Dk. Shein pia, aliwapongeza wanafunzi wa kike kwa kufanya vizuri katika
masomo yao na kueleza haja ya kufanywa utafiti ili kuweza kujua ni kwa nini
watoto wa kiume wamekwua wakiachwa nyuma.
Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kutoridhishwa na kuona kuwa
hakuna Mkoa hata mmoja uliotoa taarifa juu ya maendeleo ya skuli 19 za Sekondari za Wilaya na kueleza kuwa atakuwa
anafuatilia matokeo ya skuli hizo ambazo zimejengwa kwa gharama kubwa na
Serikali.
Sambamba na hayo, aliupongeza uongozi wa Mkoa huo kwa kuimarisha ulizni
na usalama katika kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi
na kijamii katika hali ya amani na utulivu na kuutaka uendelee kusimamia amani,
umoja na mshikamano na kutoa huduma kwa wananchi bila ya ubaguzi kwani wote ni
wamoja.
Aliitaka Mikoa yote ya Pemba iendeleze juhudi za kushajihisha ufugaji
wa samaki katika Mikoa na maeneo mbali mbali yanayoweza kuendeleza shughuli
hizo.
Dk. Shein apia, aliwataka viongozi wote wakiwemo wa Mawaziri, Wabunge,
Wawakilishi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu
Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Wadhamini, viongozi wa
Serikali, chama cha CCM, Masheha, Makamanda.
Dk. Shein amemaliza ziara yake katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba
iliyoanza tarehe 12 Agosti mwaka huu huko katika Mkoa wa Kaskanini Unguja ikiwa
na lengo la kuangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka
2015-2020 pamoja na uimarishaji wa Matawi na Maskani za CCM hapa nchini.
Post a Comment