SERIKALI YAJENGA SOKO JIPYA LA TIBIRINZI ILI WAFANYABIASHARA WAWEZE KUUDHA BIDHAA ZAO.
Zanzibar
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema
kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga soko jipya la Tibirinzi
ni kwa ajili ya wafanyabiashara kuuza bidhaa zao ili wananchi wapate huduma
wanazozihitajia bila ya kuingiza itikadi za kisiasa wala jinsia sokoni hapo.
Dk. Shein amesisitiza kuwa jengo hilo jipya la soko
lisijegeuzwa sehemu ya kufanyia siasa na badala yake lifanye kazi iliokusudiwa
kwani kwa kipindi kirefu wafanyabiashara wa soko hilo walikosa eneo la uhakika
la kufanyia biashara.
Aliyasema hayo mara baada ya kuweka jiwe la Msingi
la ujenzi wa soko jipya la Tibirinzi Chake Chake Pemba ambalo limefikia
asilimia 80 za ujenzi wake na linatarajiwa ujenzi wake kukamilika mwishoni mwa
mwezi wa Septemba mwaka huu.
Aliwataka wafanyabiashara wa soko hilo wakati litakapoanza
kazi wasigombane na kuwaeleza wanaChake Chake kuwa soko hilo ni la kiwago na la
pekee Zanzibar nzima.
Dk.Shein
alitumia fursa hiyo kuwapongeza wafanyabiashara waliotakiwa kufanyabiashara zao
katika eneo hilo kwa uvumilivu wao baada ya ufinyu wa nafasi kujitokeza katika
soko lao la mwanzo ambapo mazingira yake hayakuwa mazuri wakati walipohamia na
hatimae stahama yao imewapelekea kupata soko jipya la kisasa.
Alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua mkopo kwenye benki ya
Maendeleo ya Afrika (ADB), kwa ajili ya kujenga masoko hayo kwani Serikali
imeamua kuwasaidia wananchi wake sambamba na kutekeleza ahadi yake iliyoahidi
katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ya kujenga soko hilo.
Alieleza
kuwa kutokana na mapato yanayokusanywa na Serikali ndio sababu moja wapo
iliyopelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweza kukopeshwa na Benki
kadhaa duniani kwani inakopesheka.
Aidha, ameeleza
azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuijenga upya barabara ya kutoka
Chake kupitia Ziwani hadi Wete na ile ya kutoka Chake Chake hadi Wete sambamba
na kuitia lami hivi karibuni barabara ya Ole-Pujini hadi Kengeja.
Alisisitiza
kuwa lengo ni kuibadilisha Zanzibar na katika kipindi cha miaka mitatu katika
uongozi wake yatafanywa yale yote yalioahidiwa na yale yasioahidiwa kwa azma
ile ile ya kuwapelekea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar.
Nae
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Vikosi
Maalum vya SMZ Haji Omar Kheir alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Saba
imedhamiria kuwasaidia wananchi wake katika kujikwamua na umasikini wa kipato.
Pia,
alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kuijenga barabara
inayopita mbele ya soko hilo pia, hivi karibuni katika Bajeti yake ya mwaka huu
itaijenga barabara kutoka Msingini kuelekea Miembeni.
Mkuu wa
Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa
kupata maendeleo makubwa katika Mkoa huo na kutumia fursa hiyo kueleza historia
ya soko hilo jipya hadi kupewa jina la soko la Qatar jina ambalo Dk. Shein alisema
si busara kuitwa soko hilo na liitwe jina lake la soko la Tibirinzi.
Mratibu kutoka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kupitia
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini (MIVARP) alieleza kuwa ujenzi wa soko hilo utagharimu TZS milioni
972.2.
Mratibu huyo alisema kuwa jumla ya vibaraza 76 vya wafanyabiashara
vimejengwa katika soko hilo sambamba na kuwepo chumba maalum cha barafu pamoja
na mtambo maalum wa kutengeneza vinoo vya barafu 125kg kwa saa sawa na tani 6 za
barafu ambamo mtawekwa samaki, mbogamboga, nyama na matunda mengine.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo katika soko hilo kutakuwa na umeme wa
uhakika pamoja na jenereta la hakiba lenye KVA 20.
Mapema Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya ZECCON Ali Mbarouk inayojenga
soko hilo alieleza kuwa ujenzi wa soko hilo lenye ghorofa moja ni soko la pekee
hapa Zanzibar ambalo litakuwa na mtambo na chumba maalum cha kutengenezea
barafu.
Post a Comment