SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMELENGA KUIMARISHA ZAO LA KARAFUU PEMBA
Pemba
Rais wa Zanzibar Dr.Ali Muhamed Shein akizindua zoezi la uchumaji wa karafuu katika shehia ya kifundi wilaya ya micheweni mkoa wa kaskazini Pemba |
PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa lengo la
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kuliimarisha zao la karafuu ni
kuwaneemesha wakulima wa zao hilo na kuwafanya wawe na maisha bora zaidi kuliko
ilivyo sasa.
Amesema mipango ya kuliongezea thamani zao hilo
pamoja na kuyatambua mashamba ya Serikali inalenga kuwaongezea kipato wananchi
pamoja na kuwaweka utaratibu mzuri ambao baadae utawafanya wanaoyatumia vyema
na kwa uadilifu mashamba hayo kuweza kumilikishwa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kushiriki
kikamilifu katika shughuli za uchumaji na uchambuaji wa karafuu huko katika
kambi ya Karafuu ya Mshashani ya mkulima Mohammed Kai Bakari iliyopo Kifundi,Wilaya
ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema utaratibu wa sasa ambapo wakulima wa karafuu
wanauza karafuu zao Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) kama zilivyo baada ya
kukaushwa na ZSTC kuuza kwenye soko la dunia, haziipi faida kubwa serikali wala
mkulima kuliko ambavyo zao hilo lingeongezwa thamani.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein amesisitiza kuwa
tafiti zitaendelea kufanywa kwa lengo la kuliongezea thamani zao hilo la
karafuu na kuna haja ya wanasayansi waongeze kasi katika kuliongezeza thamani
zao hilo.
Aidha, amesema mchakato wa sasa ambao serikali
unaendelea nao wa kuyatambua mashamba yake hatimaye utaweka utaratibu mzuri wa
kuwamilikisha wakulima wanaoyatumia vizuri.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imefanya uwamuzi wa makusudi wa kuliongezea bei zao hilo kwa lengo la
kulipa heshima zao la karafuu.
Aliongeza kuwa Serikali haina nia wala lengo la
kuwanyanganya wakulima mashamba ya karafuu kama inavyoelezwa na baadhi ya watu
wachache bali ina mpaongo wa kuyatambua mashamba yake yote ya karafuu pamoja na
eka za serikali.
Dk. Shein alieleza kuwa kila mwenye haki ya kupewa
shamba ama heka atapewa kwa taratibu zitakazopewa na wale wenye kuyashughulikia
mashamba hayo hivi sasa watapewa kipaumbele.
Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
Hamad Rashid Mohamed alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kushiriki vyema
katika shughuli ya uchumaji na uchambuzi wa karafuu.
Aliongeza kuwa ukulima wa zao la karafuu ni mgumu
hivyo hatua za serikali za kuwaongezea wakulima beo za zao hilo na kutoa agizo
kuwa asilimia 80 ya bei ya dunia walipwe wakulima ni mfano mzuri wa kuonesha
kuwa Rais Dk. Shein na Serikali anayoiongoza inawajali wakulima.
Mapema Dk. Shein alipata maelezo juu ya ukodishwaji
wa zao hilo la karafuu ulioanza tarehe 5 mwezi huu na tayari mashamba 100
yameshakodishwa yenye thamani ya TZS 158.9.
Shamba la mzee Mohammed Bakari Kai lima mikarafuu
125 bado halijakodoshwa lakini wakati ukifika wa ukodishwaji kipaumbele
kitawekwa kwa msimamizi wa shamba hilo ambaye ni mkulima maarufu na mwenye sifa
za kilimo ambaye aliwahi kupewa zawadi ya mkulima bora hapo
mwaka juzi.
Balozi Ali Karume ambaye ni Kaimu Waziri wa Bishara,
Viwanda na Masoko alieleza haja ya kulithamini zao hilo kwani ni zao la uchumi
hapa nchini.
Nae mkulima huyo Mohammed Kai alitoa pongezi kwa
Rais Dk. Shein kwa hatua yake ya kufika katika shamba na hatimae katika kambi
yake na kujionea shughuli za kambini hapo na kuungana na wakulima kwa kuchambua
karafuu.
Mkulima huyo alieleza anavyofarajika na juhudi za
Dk. Shein chini ya Serikali anayoiongoza katika kuliimarisha zao hilo la
karafuu huku akieleza uzoefu wake katika kilimo cha karafuu pamoja na zawadi
alizowahi kupewa kutokana na ukulima wake.
Post a Comment