ZAID YA TSH MILIONI 300 ZAKUSANYWA KWA AJILI YA MFUKO WA MAENDELEO YA UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA.
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein, amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT), katika kuuimarisha umoja huo na kusisitiza kuwa kuna kila sababu ya
kuendelea kuunga mkono kwa nguvu zote ili uzidi kupata mafanikio.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya chakula cha hisani cha
kuchangia mfuko wa Maendeleo ya Umoja wa Wanawake Tanzania, hafla iliyofanyika
katika ukumbi wa Baraza la
Wawakilishi la zamani, kikwajuni mjini Unguja.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
Kamati iliyoratibu shughuli hiyo chini ya Mwenyekiti wake Dk. Maua Abeid
Daftari na Makamo wake Mahmoud Thabit Kombo kwa kufanikisha hafla hiyo na
kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.
Katika hotuba yake fupi mara baada ya
harambee hiyo, Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na harambee hiyo
ilivyoendeshwa vizuri sambamba na mnada wa vitu mbali mbali zikiwemo picha za
kuchora kwa mkono ikiwemo picha ya Rais Dk. Shein na ile ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Aliwapongeza waalikwa kwa kuchangia na
kueleza kuwa wamethitisha usemi usemao ‘kutoa ni moyo na si utajiri’ huku
akiamini kuwa dhamira ya Umoja huo itafikiwa kutokana na malengo yao ya
kuchangisha milioni 300 ambapo baada ya harambee hiyo fedha zilizopatikana
zilivuka kiasi hicho za fedha.
Akitangaza fedha zilizopatikana katika michango
ya hafla hiyo Dk. Shein alizitaja kuwa ni TZS milioni 300,752,000 ambapo fedha
zilizopatikana katika harambee kabla ya kuingiza mchango wake zilikuwa ni TZS 290,752,000
na baada ya yeye pamoja na Mama Shein kuchagia milioni 10 taslim zilifikia
kiwango hicho na kuvuka lengo lililokusudiwa na Umoja huo za kupata milioni 300
katika harambee hiyo.
Akichanganua fedha hizo, Dk. Shein alisema
kuwa katika mnada wa vitu mbali mbali vilivyouzwa ukumbini hapo fedha
zilizopatikana ni TZS 69,600,000 ambapo michango iliyopitia Benki pamoja na fedha
taslim ni TZS 221,152,000.
Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa (UWT) kwa
upande wa Zanzibar Tunu Juma Kondo alimpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kuwajali
wanawake sambamba na kuwaunga mkono katika harakati zao za kujiletea maendeleo.
Kondo alisema kuwa hatua yake hiyo ni
muendelezo wa nia yake njema ya kuona wanawake wanafanikiwa katika kujiletea
maendeleo huku akitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa jinsi Dk. Shein
anayotekeleza kwa vitendo tena bila ya ubaguzi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015-2020.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza lengo
lao la kukusanya TZS milioni 300 katika harambee hiyo ili ziweze kuchangia
katika mfuko wao wa maendeleo.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya
shughuli hiyo, Dk. Maua Abeid Daftari, ambaye pia ni Mshauri wa Rais Pemba
alitoa pongezi kwa niaba ya Kamati yake kwa miongozo na busara walizozipata
kutoka kwa Dk. Shein ambazo zimeweza kuwafikisha katika malengo
waliyoyakusudia.
Aliongeza kuwa jumuiya ya UWT imekuwa na
mapenzi makubwa kwa Dk. Shein kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi
wote bila ubaguzi hatua inaonesha kuwa mbali ya wanawake wa Tanzania na hata
wanaume wa Tanzania nao wanaridhika na uongozi wake na kuahidi kuendelea
kumuunga mkono.
Aidha, Dk. Daftari alieleza kuwa Umoja huo
utaendelea kumuunga mkono Dk. Shein kwani wanaridhika na utendaji wake wa kazi
huku akitoa pongezi kwa Mama Mwanamwema Shein kwa kuendelea kuunga mkono Umoja
huo kwa hali na mali.
Akitoa neno la shukurani Katibu Mkuu wa UWT Amina Makilagi
aliwahakikishia wachangiaji wote waliouchangia Umoja huo katika hafla hiyo kuwa
fedha zilizopatikana zitafanyiwa yale yote yaliokusudiwa.
Katika hafla hiyo, kundi la Taraab la Culture lilitoa burudani ya pekee
kwa nyimbo zake mbali mbali zikiwemo nyimbo laini sambamba na zile za asili
zilizoipelekea hadhira kushindwa kutulia katika viti vyao na hasa pale ilipoimbwa
nyimbo ya “Mpewa hapokonyeki”.
Post a Comment