DR SHEIN AZITAKA NCHI ZA UMOJA WA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKAKUDHIBITI UKATISHAJI WA FEDHA HARAMU.
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amezitaka nchi za Umoja
wa Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu
(ESAAMLG) kufanya kazi kwa karibu na Jumuiya hiyo ili ziweze kupambana na uharamia
huo unaoathiri sekta za kiuchumi na maendeleo kwa nchi wanachama.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort, Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati akifungua
Mkutano wa Umoja wa Nchi za Umoja wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG)
wenye mada kuu za udhibiti katika utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa
ugaidi zitajadiliwa.
Alisema kuwa kuwepo kwa
mfumo wa fedha haramu kunaathiri sana juhudi za Serikali katika upatikanaji wa
rasilimali fedha ambazo zinaweza kutumika vizuri na kuelekezwa katika
utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa nchi za Umoja huo.
Alieleza kuwa Jumuiya
hiyo ina jukumu kubwa la kupambana na vitendo vya utakasishaji wa fedha haramu pamoja
na kudhibiti vitendo vya kuziwezesha kifedha taasisi na vikundi
vinavyojishughulisha na masuala ya kigaidi.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa ipo haja kwa nchi wanachama kuweka mikakati imara ya kuweza kufahamu
uhusiano uliopo baina ya utakasishaji wa fedha haramu na masuala ya kigaidi na
kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika kudhibiti vitendo
hivyo.
Aliongeza kuwa iwapo
nchi zote wanachama 18 wa Jumuiya hiyo zitaelekeza nguvu na juhudi kubwa katika
vitendo hivyo basi vitaweza kupata mafanikio yaliokusudiwa sambamba na malengo
ya Jumuiya hiyo.
Alieleza kwamba nchi za
ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini zingeelekeza nguvu zake vizuri na kutumia
vyema rasilimali zake na kudhibiti vitendo hivyo zingeweza kwenda katika kasi
sawa na nchi za Malaysia, Singapore, Malta na Korea Kusini ambazo zimepata
uhuru katika wakati mmoja na nchi za Jumuiya hiyo.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alieleza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo zinakabiliwa na changamoto
kadhaa zikiwemo rushwa, ukwepaji wa kodi, usafirishaji wa fedha nje ya nchi,
biashara ya dawa za kulevya,uharibifu wa mazingira, utengenezaji wa fedha
kinyume na sheria, vitu bandia pamoja na udanganyifu katika masoko ya hisa na
changamoto nyenginezo
Aliongeza kuwa ipo haja
ya kuungana na kuwa na sheria na mikakati madhubuti itakayowezesha nchi
wanachama kuhakikisha kuwa mapato yanayopatikana kutokana na vitendo hivyo haramu
yanadhibitiwa na kuhakikisha hayatumiki katika kuendeleza vitendo hivyo.
Aidha, Dk. Shein alieleza
juhudi zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana na vitendo hivyo ikiwa ni
pamoja na kupambana na rushwa, utakasishaji wa fedha haramu, ugaidi na masuala
mengine yalio kinyume na taratibu za nchi kwa kutunga sheria mbali mbali kwa
ajili ya kudhibiti vitendo hivyo.
Alizitaja baadhi ya
miongoni mwa sheria hizo ikiwa ni pamoja na Sheria ya kudhibiti vitendo vya
ugaidi, Sheria ya kudhibiti utumiaji mbaya wa mitandao, Sheria ya kudhibiti
dawa za kulevya, Sheria ya kupambana na kudhibiti rushwa na sheria nyenginezo.
Vile vile, Dk. Shein
alisema kuwa Tanzania imeweza kuanzisha taasisi mbali mbali za kudhibiti vitendo
hivyo ikiwemo Taasisi katika Mahakama inayohusiana na kupambana na Rushwa na
Uhujumu Uchumi, Taasisi za kupambana na Dawa za kulevya na nyenginezo na
kuzitaka nchi wanachama kuzijengea uwezo taasisi kama hizo katika nchi zao.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliwahakikishia wajumbe hao wa mkutano huo kuwa Tanzania itaendelea kutoa
ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha Umoja huo unaendelea kutekeleza
majukumu yake ipasavyo na kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kutoa pongezi kwa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake katika Umoja huo ambaye
pia, ni Waziri wa Fedha na Uchumi wa Jamhuri ya Zimbwabwe Patrick Chinamasa
aliyemaliza muda wake mwezi Agosti mwaka huu
na nafasi yake kushikwa na Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwakaribisha Zanzibar wajumbe hao wa mkutano na kuwataka kuitembelea na
kuona mazingira yake sambamba na vivutio mbali mbali vilivyopo.
Nae Waziri wa Fedha na
Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango
alizihakikishia nchi wanachama za Umoja huo kuwa Tanzania itauendeleza kwa
nguvu zake zote umoja huo ikiwa ni pamoja na kuongeza ushirikiano zaidi kati ya
nchi wanachama pamoja na kuongeza ofisi sambamba na kuwaimarisha watendaji wake.
Mapema Waziri wa Fedha
na Maendeleo ya Uchumi wa Zimbabwe Patrick Chinamasa alizitaka nchi wanachama
kuongeza nguvu katika kutoa michango yao pamoja na kuziimarisha taasisi za
kupambana na kudhibiti utakasishaji wa Fedha haramu katika nchi hizo ili Umoja
huo uzidi kuimarika na kuleta manufaa yaliokusudiwa.
Waziri Chinamasa
alieleza kuwa katika mkutano huo mbinu na mikakati mbali mbali itakayosaidia
kudhibiti utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi utajadiliwa, hatua
ambayo italeta matokea mazuri na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kufikia
maendeleo yanayotarajiwa katika nchi wanachama.
Tanzania kwa hivi sasa
ni Mwenyekiti wa Umoja huo ambayo ni miongoni mwa waanzilishi wa Umoja huo
ambao kwa hivi sasa una wanachama 18 kutoka wanachama 7 waanzilishi baada ya
kupokea kutoka Jamhuri ya Zimbabwe iliyomaliza muda wake Agosti 2017.
Post a Comment