SHIRIKA LA CHAKULA NA KILIMO LA UMOJA WA MATAIFA (FAO) LAPONGEZWA
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa
(FAO) kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa
nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati
alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la
Umoja wa Mataifa (FAO), Dk. Jose Graziano da Silva, ambaye amefika Zanzibar kwa
lengo la kuongeza mashirikiano baina ya Shirika hilo na Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo,
Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa FAO ni miongoni mwa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa yalio na historia kubwa katika kuisaidia Zanzibar katika sekta
ya kilimo pamoja na mazao yanayohusiana na chakula.
Aliongeza kuwa FAO
imeweza kutoa misaada mbali mbali ya kuendeleza sekta ya kilimo hapa Zanzibar na
kumueleza Mkurugenzi Mkuu huyo jitihada za wananchi wa Zanzibar katika
kuliendeleza zao la mwani na kusisitiza haja kwa Shirika hilo kuiunga mkono
Zanzibar katika kuhakikisha kilimo hicho kinawanufaisha wakulima wake.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitoa pongezi za pekee kwa Shirika hilo kwa ushirikiano wake mkubwa
unaotoa katika kupambana na athari za kilimo zinazosababishwa na wadudu
waharibifu wa matunda ikiwa ni pamoja na utafiti wa maradhi ya zao la mwani.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Mkurugenzi Mkuu huyo juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya kilimo na uvuvi pamoja na azma ya kuanzisha viwanda
vidogo vidogo ambavyo malighafi zake zitatokana na rasiliamali za sekta hizo
ili kwa pamoja ziweze kuwa na mchango mkubwa katika soko la ajira hasa kwa vijana.
Dk. Shein alimueleza
Mkurugenzi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Wizara yake ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya kilimo,
uvuvi na uvugaji ili sekta hizo ziweze kuleta tija na kutoa ajira hasa
ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya wananchi wa Zanzibar wanajihusisha katika
sekta hizo.
Hivyo, alimshauri
Mkurugenzi Mkuu huyo kuwa katika ziara yake ijayo ni vyema akatembelea kisiwani
Pemba kwa lengo la kuangalia juhudi za wananchi wa kisiwa hicho katika
kuendeleza sekta ya uvuvi na ufugaji hasa ufugaji wa samaki.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kulipongeza Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Kilimo na
Chakula Duniani pamoja na kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wake Dk. Graziano da Silva
kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kusaidia katika kuhakikisha sekta ya
kilimo inazidi kuimarika.
Nae Dk. Graziano da
Silva alimuhakikishia Dk. Shein pamoja na kuihakikishia Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono na kuisaidia Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya Kilimo na kulipokea wazo la Rais Dk. Shein la kuwajengea
uwezo kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wa kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo Kizimbani.
Mkurugenzi Mkuu huyo alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa uongozi wa Wizara
husika ya Kilimo pamoja na ziara aliyofanya katika maeneo mbali mbali yakiwemo
mashamba ya viungo na maeneo ya utafiti Kizimbani.
Hivyo, alieleza kuwa
baada ya ziara yake hiyo ameweza kugundua utajiri mkubwa ulionao Zanzibar wa
mazao ya viungo ambayo Shirika lake la FAO litaangalia namna ya kusaidia ili
bidhaa hizo za viungo ziweze kutengenezewa dawa za tiba asilia.
Dk. Graziano da Silva
alisema kuwa umefika wakati wa kuelekeza nguvu zote katika mageuzi ya kilimo
hatua ambayo itaimarisha zaidi uzalishaji wa mazao ambayo yataimarisha sekta ya
biashara sambamba na sekta ya viwanda hapa nchini.
Dk. Graziano da Silva
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Zanzibar kwa kuendeleza ushirikiano na
uhusiano mwema uliopelekea mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo hapa nchini
kwa kuimarisha uhakika wa chakula na maendeleo ya ya sekta hiyo.
Pamoja na hayo,
Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO aliipongeza Zanzibar kwa kuendeleza na kusimamia
vyema miradi yote inayoendeshwa na Shirika hilo na kusisitiza kuwa limefarajika
na juhudi hizo na itaendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu
huyo, alimueleza Dk. Shein juhudi zinazochukuliwa na Shirika hilo la FAO katika
kuhakikisha usalama wa chakula unakuwa ni ajenda muhimu kwa nchi za bara la Afrika
kwani ni jukumu moja wapo la Shirika hilo.
Post a Comment