Header Ads

WADAU WA HAKI ZA BINADAMU WAUNGA MKONO TAMKO LA RAIS LA KUKATAA KUNYONGWA KWA WASHTAKIWA WA MAUAJI.

PEMBA
WADAU wa haki za binadamu nchini, wamesema tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: John Pombe Magufuli ya kukataa kuwanyonga washitakiwa wa mauwaji, ni hatua moja muhimu ya kueleka kuthamini haki za binadamu.
Walisema kwa muda mrefu, walikuwa wakipigia debe juu ya sheria inayowapa mamlaka Majaji kutoa huku ya kunyongwa ifutwe nchini, kutokana na kwenda kinyume na Katiba, ambapo sasa tamko la Rais linaelekea paha pazuri.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania ‘LHRC’ Dk Helen Kijo Bisimba, alisema tamko hilo amelipoeka kwa furaha na sasa atafurahi zaidi, iwapoi sheria husika nayo itafutwa.
Akizungumza na kituo kimoja na TV nchini, alisema wakati umefika sasa kwa Rais aliepo wa Tanzania, kutumia uwezo na ushawishi wake, ili sheria husika iondolewa kwenye vitabu vya sheria.
Mkurugenzi  huyo alisema, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kwenye Ibara ya 14 imeeleza wazi kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ndani ya jamii, hivyo kuwanyoga washitakiwa hadi kufa, ni kuwenda kinyume na sheria hiyo mama.
“Mimi kwa kweli nimepokea kwa furaha tamkoa la Mhe: Rais la kwamba asipelekewa orodha ya majina ya washitakiwa wanaosubiri kunyongwa, na hili sasa linatoa ishara kwamba hata sheria inaweza kufutwa hapo baadae”,alifafanua.
Katika hatua nyengine, Mkurugenzi huyo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania Helen Kijo Bisimba, alimuomba rais huyo wa Tanzania, kutoa tamko rasmi la kufutwa kwa sheria hiyo.
Nae Mwanasheria dhamana wa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaa DPP Kisiwani Pemba, Ali Rajab Ali, alisema tamko hilo la raisa ni jema, maana lilikuwa haliendani na sheria mama.
Alisema sasa kilichobakia ni kuhakikisha sheria husika nayo inafutwa ili sasa washitakiwa wapewa adhabu mbadala.
“Na sisi Zanzibar kwenye maandiko yetu ya sheria no 6 ya mwaka 2004 ya kanuni za Adhabu inawapa mamalaka majaji kutoa uamuzi wa mshitakiwa kupewa adhabu ya kifo, lakini haitekelezwi”,alifafanua.
Baadhi ya wananchi kisiwani Pemba, walisema kwa Zanzibar wakati umefika sasa, nayo kufuata nyayo hizo ili wale wanaoshitakiwa kunyongwa, wapewa adhabu mbadala ya kifungo cha maisha.
Omar Haji Makame wa Wawi Chakechake alisema, kuwanyonga watu kwa sababu yao kuwa wameua, itakuwa ni kuibua hisia za visasi, ambavyo vinaweza kuwa endelevu.
Nae Mwenyekiti wa Jumuia ya uhifadhi ya Mazingira Vitongoji Chakechake VECA Sifuni Ali Haji, alisema baada ya tamko hilo, sasa ni vyema rais akatumia mamlaka yake kuhakikisha sheria hiyo inafutwa.
Alisema kwa muda mrefu na yeye kwa nafasi yake, aliwakua akiomba kwa mamlaka husika za serikali, kuwaondolewa uwezo walionao majaji wa mahakama kuu, wa kutoa uamuzi wa hukumu ya kifo.
Nae Omar Mcha Hashim alifafanua kuwa, lazima kwa Zanzibar nayo ambayo haijawi kutekeleza adhabu ya hiyo tokea mwaka 1964, kuondoa sheria hiyo na washitakiwa kupewa kifungo cha maisha jela.
“Hata wakifunguwa miaka 30 au miaka 40 ni bora kuliko kuendelea kuwatia wasiwasi wa kunyongwa, ingawa hilo halitendeki”,alifafanua.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tokea mwaka 1994 haijawi kunyonga tena washitakiwa wanaotakiwa kunyongwa hadi kufa na sasa wakiwashikilia washitakiwa zaidi ya 400 wanaosubiri kunyongwa, ambapo kwa Zanzibar pamoja na kuwa na sheria hiyo, haijawi kunyonga tokea mwaka 1964.

No comments