Wanafunzi Skuli ya Sekondari UWELENI Watakiwa Kujisomea

WANAFUNZI wa Skuli ya Sekondari ya Uweleni Mkoani Pemba, wametakiwa
kuzidisha nguvu zao katika suala la elimu, ili kuweza kukabiliana na mitihani
yao ya taifa inayotegemewa kuanza
mwanzoni mwa wiki ijayo.
Akizungumza na wanafunzi skulini hapo,
Mkurugenzi Baraza la Mji Mkoani Rashid Abdalla Rashid, amesema wanafunzi
watakapo zidisha nguvu zao katika masomo, wataweza kukabiliana vyema na
mitihani yao na kuleta ufaulu mzuri utakaowawezesha kuingia katika vyuo mbalimbali
ndani na nje ya nchi .
Amesema ni vyema kwa wanafunzi hao kujikita katika masomo ya
Sayansi, ili waweze kukabiliana na soko la ajira na kupunguza tatizo la uhaba
wa madaktari na walimu wa masomo hayo.
Wakati huo huo, Mkurugenzi huyo ametowa ahadi kwa wanafunzi
watakaopata matokeo mazuri ya kiwango cha ‘A’ na ‘B’ ya masomo ya sayansi na
kiingereza, kuwazawadia vifaa vya kusomea vikiwemo vitabu mabuku, ada pamoja na
sare.
Katika hatuwa nyengine, aliwataka walimu wa Skuli hiyo kusomesha
kwa bidii na kuwashajihisha wanafunzi kuachana na masuala yasiyowahusu, ikiwemo
kujishirikisha na vikundi viovu.
Kwa upande wake mwalimu
Mkuu wa Skuli hiyo, Shehe Hassan Mohamed amesema, jukumu lililobakia ni la
wanafunzi wenyewe kuweza kufanya vizuri, katika kuleta ufaulu mzuri kwani walimu walikamilisha muhutasari
kwa wakati.
Post a Comment