ZAECA Yaokoa Zaidi ya Shilingi Milioni 84.7

ZAIDI ya
shilingi milioni 84.7 zimeokolewa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa
Uchumi Zanzibar (ZAECA) Kisiwani Pemba, kwa kuyaibua mashamba ya mikarafuu 30
ya Serikali, yaliyodaiwa kufichwa wakati wa zoezi la ukodishaji ulipokuwa
ukiendelea.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Chake Chake,
Mdhamini wa Mamlaka hiyo Pemba, Suleiman Ame Juma alisema, mashamba hayo
waliyafichua baada ya watendaji wake kufanya uchunguzi wa kina, wa mashamba
hayo ya mikarafuu.
Alisema kuwa, baada ya kufanya uchunguzi huo, walibaini
kwamba jumla ya shilingi milioni 84,700,000 zingepotea na kuishia mikononi mwa
wachache, ingawa walifanikiwa kuziokoa, kutokana na kufichwa kwa mashamba 30 ya
eka tatu tatu ya Serikali, katika maeneo tofauti ya kisiwani Pemba.
“Zaidi ya mashamba 30 ya mikarafuu ambayo yalionekana kama
sio ya serikali, lakini baada ya uchunguzi wetu
tumeyabaini, kwamba ni ya serikali na tumefanikiwa kuziokoa fedha hizo
baada ya kukodishwa”, alisema Suleiman.
Alifafanua kuwa, kuna mashamba yamekuwa yakifichwa na baadhi
ya watendaji au watu wa kawaida, na kuonekana kama sio ya serikali, ambapo
watendaji mbali mbali serikalini, hutumia mwanya huo kwa kuyatumia wao, jambo
ambalo ni kosa kisheria.
“Kwa kweli mashamba yanafichwa kwa lengo la kuyatumia kwa
shughuli zao binafsi, lakini tutaendelea kuchunguza, ili kuondoa suala zima la
uhujumu wa uchumi, kama moja ya kazi zetu”,aliongeza.
Alieleza kuwa, kama hadi sasa Wizara husika imeshaingiza
shilingi milioni 900.661, kwa ukodishaji wa mashamba ya serikali, basi mchango
wa ZAECA, baada ya kuyaibua mashamba hayo 30 katia ya 1,451, ni shilingi miloni
84.7, ni mchango wetu.
Alisema walizipata taarifa hizo, baada ya kuhojiana na
wananchi na wengine kufika ofisini kwao kutoa taarifa, juu ya uwepo wa mashamba
ya mikarafuu ya serikali, kwenye maeneo ambayo zoezi limeshapita.
Tayari mashamba ya mikarafuu ya eka tatu tatu 1,451 yameshakodishwa
na wizara ya Kilimo, Maliasiali, Mifugo na Uvuvi Pemba, na laiti kama waliokodi
wengeshalipa fedha zote hizo, serikali ingejipatia wastani wa zaidi ya shilingi
bilion 2.393.
Ingawa hadi sasa katia fedha hizo ziliotarajiwa kupatikana,
hadi Oktoba 17, ni shilingi bilioni 1.492 zilizokuwa hazijalipwa na wanchi
mbali mbali waliokodia mashamba ya mikarafuu ya serikali kisiwani Pemba.
Zoezi la ukodishaji
wa mashamba ya mikarafuu kisiwani Pemba, lilianza mwezi Julai mwaka huu, ambapo
jumla ya mashamba 1,451 yalishakodishwa, kati ya mashamba 1,525 yaliotarajiwa
kuibuliwa kabla ya kuanza kwa zoezi la ukodishaji.
MWISHO.
Post a Comment