DC Miecheweni Alivyofungua Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Wanafunzi Juu ya Elimu ya Afya ya Uzazi na Ushiriki Katika Uandaaji wa Vipindi Vya Redio
Mkuu wa wilaya ya
micheweni Salama Mbarouk Khatib amewataka wanafunzi wanaoshiriki mafunzo ya
Afya ya uzazi kuwa makini wakati wa mafunzo watakayo yapata kutoka Shirika la
Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ili kuifikisha elimu hiyo kwa wanafunzi
wenzao na jamii kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati
akifungua mafunzo hayo ya siku sita ya kuwajengea uwezo wanafunzi uelewa wa
elimu ya jinsia, afya ya uzazi na ushiriki katika uandaaji wa vipindi vya redio
katika sikuli ya Chwaka Tumbe wilaya ya Micheweni.
Amesema endapo
wanafunzi watayasikiliza mafunzo hayo kwa umakini watakuwa walimu wa kutoa
elimu juu ya masuala mbalimbali ikiwemo afya ya uzazi.
“Endapo kama
mutayazingatia mafunzo haya yatawasaidia sana katika kupambana na masuala ya
udhalilishaji lakini pia suala la UKIMWI na kuondokana na Ndoa za Utotoni.”
Alisema Salama.
Mkuu huyo wa wilaya
ameyataja baadhi ya masuala ambayo yamekuwa yakiirejesha nyuma jamii ya
Micheweni kuwa ni kuendelea kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji pamoja na elimu
ndogo ya Afya ya uzazi kwa vijana.
Aidha ametumia nafasi
hiyo kulipongeza shirika la, UNESCO kwa juhudi walizo zifanya na kuamua kutoa
elimu katika wilaya ya micheweni kuhusiana na suala zima la Afya ya Uzazi.
“nipende kuchukua
nafasi hii kuwapongeza UNESCO kwa maamuzi ya kuichagua Micheweni kwaajiri ya
kuja kutoa elimu hii muhimu kwa vijana wetu, niombe na mashirika mengine yaige
mfano huu.” Alisema mkuu huyo.
Katika hatua nyingine
bi Salama amewataka maafisa waandamizi kutoka wizara ya elimu kuvitumia vyombo
vya habari ikiwemo kituo cha redio jamii micheweni ili kutoa ripoti za masuala
mbalimbali yanayohusu elimu.
Kwa upande wake kaimu
afisa elimu wilaya ya micheweni, Mwalimu Bakari Khamis Juma, amewataka
wanafunzi hao kutoa ushirikiano kwa wawezeshaji ili waweze kujifunza mambo
mengi zaidi.
Mafunzo ya kuwajengea
uwezo wanafunzi kushiriki katika uandaaji wa vipindi vya redio na elimu ya afya
ya Uzazi yanawashirikisha wanafunzi kutoka shule Nne za wilaya ya Micheweni, Walimu
Pamoja na Wazazi.
Post a Comment