Rais Dk. Shein Afungua Milango ya Maendeleo Uarabuni
ZANZIBAR na Sharjah zimekubaliana
kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao uliopo katika kuimarisha sekta
mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu na biashara,
Katika mazungumzo yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Makaazi ya Mtukufu Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al Qasimi mjini
Sharja, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein na kiongozi huyo wote kwa pamoja walisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano
na ushirikiano uliopo kwa lengo la kuimarisha sekta hizo muhimu za maendeleo.
Rais Dk. Shein kwa upande wake
alimpongeza Dk. Sultan kwa hatua zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuimarisha miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji.
Pamoja na hayo, viongozi hao
walizungumza jinsi ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuimarisha
sekta ya elimu hasa ikizingatiwa kuwa Sharjah imeweza kupata mafanikio katika sekta hiyo kutokana
na kuwa na miundombinu mizuri ya elimu vikiwemo vyo vikuu.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa
Sharjah kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika sekta ya elimu kupitia Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), jambo ambalo Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al
Qasimi ameliunga mkono.
Pia, viongozi hao kwa pamoja,
wameeleza namna ya pande mbili hizo kushirikiana katika sekta ya biashara hasa
ikizingatiwa kuwa kuna bidhaa ambazo ziko Zanzibar na zinatumika sana nchini
Sharjah vikiwemo viungo ambapo nchi hiyo wamekuwa wakinunua kutoka nchi za
mbali ikilinganishwa na masafa kati ya Zanzibar na Sharjah.
Dk. Shein, pia alitumia fursa hiyo
kumueleza Dk. Sultan hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya utalii zikiwemo uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambapo
tayari serikali imejenga ukuta wa kuzuia athari za maji ya bahari katika eneo
la Mizingani kuelekea katika bustani ya Forodhani.
Kwa upande wake Dk. Sheikh Sultan
nae alimueleza namna Sharjah ilivyokuwa na uhusiano na ushirikiano na Zanzibar
kwa muda mrefu jambo ambalo amehakikisha ataliendeleza na kuliimarisha kwa
lengo na manufaa ya pande zote mbili.
Pia, Dk. Sheikh Sultan alimuleza
Rais Dk. Shein namna Sharjah ilivyopiga hatua katika sekta ya elimu sambamba na
inavyotoa fursa za ufadhili wa masomo na kusisitiza kuwa kuna kila sababu na Zanzibar nayo ikafaidika na fursa
hizo.
Aidha, Dk. Sultan alimueleza Dk.
Shein fursa mbali mbali za kibiashara zilizopo Sharjah na kusisitiza haja ya
kuwepo mashirikiano kati ya pande mbili hizo ili sekta hiyo ilete manufaa kwa
pande zote mbili hizo.
Katika kuendeleza na kukuza sekta
ya biashara na utalii kati nchi mbili hizo, Dk. Sultan alimueleza Rais Dk.
Shein umuhimu wa kuwepo usafiri wa ndege wa moja kwa moja kati ya Zanzibar na
Sharja na kusisitiza kupitia Shirika la ndege la Sharjah hilo atahakikisha
analiweka katika vipaumbele vyake katika kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo.
Katika ziara yake mjini Sharja Dk.
Shein alipata fursa ya kutembelea eneo la shughuli za uvuvi la ‘East Fishing
Processing LLC”, lililoko Al Jurf katika
eneo la Ajman na kupata maelezo juu ya namna
ya eneo hilo lenye kiwanda kikubwa cha kisasa cha samaki jinsi
kinavyosarifu na kuhifadhi samaki pamoja
na kuwaweka katika mfumo maalum wa kwa ajili ya kuuzwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni hiyo inayolishirikisha kundi la Kampuni ya THOMSUN, K.V. Thomas
alimueleza Rais Dk. Shein namna na kiwanda hicho kinavyosarifu samaki wa aina
mbali mnali wakiwemo kamba kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Tanzania.
Dk. Shein kwa upande wake
alipendezewa na namna kiwandaa hicho kinavyofanya kazi na kutokana na juhudi
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya
uvuvi na viwanda vya samaki pamoja na azma ya kuanzisha Kampuni ya Uvuvi, Rais
Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja ili Zanzibar
ipate kupanua wigo katika sekta hiyo.
Kutokana na kiwanda hicho kutumia
teknolojia ya kisasa katika kusarifu samaki wa aina mbali mbali pia, soko la
ajira limeonekana kuchukua fursa yake kutokana na kuajiri vijana wengine hatua
ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kupambana na changamoto
iliyopo katika suala zima la ajira.
Wakati huo huo, Dk. Shein na
ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein walitembelea katika shamba la ngombe wa maziwa la Al Rawabi,
ambapo pia eneo hilo lina viwanda vya vinywaji vya matunda pamoja na bidhaa
nyengine zinazotokana na maziwa.
Akiwa katika eneo hilo la Al
Rawabi, Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wake ambapo Mkuu wa
Kampuni inayosimamia Shamba hilo Abdalla Eleweis alimkaribisha Dk. Shein na
ujumbe wake na kumueleza namna eneo hilo linavyofanya shughuli zake za ufugaji
wa ngombe pamoja na uendelezaji wa viwanda vya matunda.
Nae Meneja Mkuu wa Shamba hilo Dk.
Ahmed Eltigani Al Mansour alimueleza Rais Dk. Shein na ujumbe wake jinsi ya
shamba hilo linavyofuga ngombe kwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwemo
kuwawekea viyoyozi na mafeni maalum kutokana na mazingira ya hali ya hewa ya
ukanda huo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Ahmed
shamba hilo lina ngombe 12,500 ambapo kwa kila ngombe mmoja kwa siku hutoa lita
60 za maziwa na kutoa lita 250,000 kwa siku huku akitumia fursa hiyo kueleza
siri ya mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na utafiti mkubwa walioufanya kabla ya
kuazisha ufugaji huo.
Dk. Ahmeda alieleza kuwa ufugaji
wanaoufanya ni ufugaji bora duniani na pia ni eneo lililopata mafanikio makubwa
ikifananishwa na ufugaji unaofanyika katika maeneo mbali mbali zikiwemo nchi za
Afrika na hata nchi zilizoendelea ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wingi.
Akimaliza ziara yake katika eneo
hilo, Rais Dk. Shein aliuhakikishia uongozi wa Al Rawabi kuwa Zanzibar itakuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha mashirikiano yanakuwepo katika sekta hiyo ya
ufugaji ikiwa ni pamoja na kupanua wigo na kujifunza jinsi ya mafanikio hayo
yalivyopatikana.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Post a Comment