'Hakuna Maendeleo Bila kuwepo kwa Walimu Bora'- Rais Dk. Shein
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa bila ya
kuwa na walimu wenye dhamira ya dhati ya kufundisha katika ngazi zote za elimu itakuwa
ni ngumu kupata maendeleo ya kweli yanayokwenda sambamba na mabadiliko na
mwelekeo wa karne ya 21.
Dk.
Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la zamani la Wawakilishi,
Kikwajuni mjini Unguja katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa
Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU).
Katika
hotuba hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa
hakuna mtaalamu duniani ambae hakuandliwa na mwalimu kwa njia rasmi au isiyo
rasmi, na kuwaeleza walimu hao jukumu kubwa walionalo katika kuitoa Zanzibar
hapa ilipo na kuipeleka kule ambako wananchi wanataka kwenda.
Dk.
Shein alieleza kuwa mataifa mengi yaliyopiga hatua za haraka katika karne ya
21, yaliweka mkazo kwa kuwekeza katika elimu kwani fedha pekee yake haiwezeshi
Taifa lolote lile kupata wataalamu wazalendo inaowataka.
“Wataalamu
wazalendo wahitaji kutayarishwa na walimu wazalendo, kuanzia ngazi ya msingi
hadi Chuo Kikuu”,alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimepelekea kuanzishwaa vyuo vikuu
ambavyo tayari vipo vitatu vinavyoendeshwa na wataalamu wazalendo ambapo kwa
mwaka huu wa masomo uliomaliza, vyuo hivyo vimeweza kutoa jumla ya wahitimu
4,287.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na walimu
wote kwa matokeo mazuri yaliopatikana kwa niaba yake na Serikali kwa jumla
kutokana na ufaulu wa wanafunzi wote waliofanya mitihani ya Taifa wakiwemo wa
darasa la nne, darasa la sita, kidato cha Pili, Kidato cha Nne na Kidato cha
Sita.
Hata
hivyo, kutokana na ufaulu wa kidato cha nne kushuka, Dk. Shein aliuagiza
uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali uandae mkutano maalum na walimu
wa skuli saba za sekondari za Zanzibar zilizomo katika orodha ya skuli 10
zilizofanya vibaya kwa Tanzania nzima mwaka 2017.
Alieleza
kuwa katika mkutano huo wajadili sababu zilizopelekea skuli hizo zifanye vibaya
sambamba na kuandaa mkakati maalum ili kuondokana na tatizo hilo na kumtaka
Waziri wa Wizara hiyo kuongoza mkutano huo ambapo alisikitishwa na hali hiyo na
kueleza kuwa wanafunzi wa Zanzibar wanaweza kufanya vizuri iwapo watapata
maelekezo mazuri kutoka kwa walimu wao kwani Zanzibar ina historia nzuri
kielemu.
Dk.
Shein alisema kuwa Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya elimu kwa kila mwaka,
ili sekta hiyo izidi kuimarika ambapo TZS Bilioni 120.726 ziliingiziwa Wizara
hiyo mnamo mwaka 2015/2016,TZS Bilioni 133.501 mwaka 2016/2017 na TZS Bilioni
197.290 mwaka 2017/2018 na kuahidi kuongeza zaidi kwa mwaka 2018/2019.
Alieleza
kuwa wapo baadhi ya walimu wanaharibu fani ya uwalimu ambayo ni fani yenye
heshima kubwa kutokana na tamaa zao na wale ambao wanaingiza siasa katika fani
hiyo huku akieleza kukerwa na tabia ya baadhi ya walimu kufanya biashara ya
urojo na biskuti skuli huku wakisingizia kushuka kwa elimu wakati wao ndio
chanzo.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuwa katika kuongeza ufanisi wa maendeleo ya skuli suala la
ukaguzi wa skuli na walimu ni muhimu lakini kwa bahati mbaya suala hilo
limekuwa halifanywi vizuri.
Pia, Dk.
Shein alieleza kuwa wakati alipofanya ziara za Mikoa mnamo mwezi Agosti 2017
aliagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ushirikiane na
viongozi wa Mikoa na Wilaya katika kuzifanyia kazi changamoto ya kuwepo kwa utoro
uliokithiri wa walimu na wanafunzi lakini hadi leo hajapelekewataarifa yoyote.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein aliwaeleza walimu hao kuwa katika ombi lao la kuwapatia
posho walimu wakuu la asilimia 50 Serikali haiwezi kufanya hivyo hadi pale
walimu hao nao kwa upande wao wajue wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao.
Pia,
Rais Dk. Shein aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
kuhakikisha inashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango inawalipa walimu
malimbikizo yao yote wanayodai ili mwakani kwenye mkutano kama huo wasijekuleta
madai hayo na badala yake waelezee mafanikio na mambo mengineyo kuhusu chama
hicho cha walimu Zanzibar na sio kudai fedha zao za malimbikizo.
Kuhusu
Muundo wa Utumishi wa Wizara ya Elimu, Dk. Shein aliitaka wizara hiyo kwa
kushirikiana na Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwarudishia
walimu na kuhakikisha wanalipwa haki zao zote pamoja na kuziangalia Wizara
nyenginezo zote kwani tayari ameshatoa agizo ya kufanyiwa kazi suala hilo.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha wanakutana na uongozi
na wajumbe wa chama hicho angalau mara mbili kwa mwaka na katika mkutano huo
watumie fursa hiyo kujadili na kupokea maoni kutoka kwa chama hicho yenye
mustakbali wa kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Nae
Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Mahamoud Thabit Kombo, ambaye pia, ni Waziri wa
Afya alieleza kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea kuwepo kwa changamoto
katika elimu ikiwemo ya wingi wa wanafunzi madarasani ni kuongezeka kwa idadi
ya watu Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa katika nchi za Afrika, idadi ya watu Zanzibar
imekuwa ikiongezeka kwa asilimia kubwa.
Nae Rais
wa Chama hicho Mwalimu Seif Mohamed alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Shein kutokana
na juhudi za makusudi anazozichukua katika kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa
Serikali wakiwemo walimu.
Mapema
Katibu Mkuu wa Chama hicho cha Walimu Zanzibar Mussa Omar Tafurwa alisoma
risala ya Walimu na kueleza mafanikio iliyoyapata Jumuiya hiyo sambamba na
changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kueleza haja ya walimu wakuu kupewa
posho la asilimia 50 ya mishahara yao, madai yao na malimbikizo wanayodai
pamoja na mambo mengineyo.
Post a Comment