Header Ads

KATIBU MPYA WA IDARA YA ITIKADI NA UENEZI CCM ZNZ AKABIDHIWA OFISI LEO



Chama Cha Mapinduzi Logo.png 
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine Peter Nao,ametaja kipaumbele chake ambacho anatarajia kuanza nacho katika utendaji wake ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), kuwa atatekeleza kwa vitendo Ibara ya 5 ya Katiba ya Chama ya mwaka 1977.
Amesema idara hiyo inawajibu wa kutekeleza ibara hiyo inayoelekeza kufanya kazi ya kuhakikisha CCM inashinda katika kila uchaguzi na kwamba ndio sehemu muhimu ya Chama kuwa na mafanikio kisiasa.
Hayo ameyasema wakati akikabidhiwa rasmi Ofisi, Kisiwandui na aliyekuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM, Zanzibar, Waride Bakari Jabu,ambaye ni Mjumbe wa Halimashauri Kuu ya Chama (NEC).
Katibu huyo amewakumbusha watumishi hao wa Idara hiyo kuwa wanatakiwa kutambua kuwa wako kwenye hatua ya kuhakikisha wanatekeleza ibara hiyo ya Tano na si vinginevyo.
Katika maelezo yake hayo Katibu huyo ameongeza kuwa Ibara hiyo inaeleza wazi na kutaka kuwa kila Uchaguzi ukifika CCM inashinda katika serikali za mitaa hadi serikali kuu na kwamba kazi ya Chama cha siasa ni kushinda na kushika Dola.
"Tuko hapa katika kutekeleza ibara hii ya tano na kuwa lengo kuu ambalo linatukutanisha ni kukipigania Chama chetu kishinde kwa kila Uchaguzi.
Pia namshukuru sana Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuniamini na akanichagua katika nafasi hii "alisema Katibu.
Mbali na hilo, Katibu huyo amemshauri Katibu mstaafu wa Idara hiyo Bi. Waride kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa Idara na Chama kwa ujumla.
"Kuondoka kwako hapa usinifungie milango bado ninakuitaji hii namna ya utaratibu wa chama chetu katika kuhamishana mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na ifahamike kuwa bado una nafasi kubwa ya uongozi tena ya kimaamuzi ya juu ya chama bado tutakuhitaji kwa namna moja ama nyingine,"amesema.
Amesema anatarajia kuendeleza mambo mema yaliofanywa na mtangulizi wake huku akibuni mikakati mipya itakayosaidia kurahisisha utendaji wa shughuli za Chama na Idara kwa ujumla.
Naye aliyekuwa Katibu wa Idara hiyo Waride amesema katika kipindi cha muda wake wa kufanya kazi kwenye idara hiyo alifanya jitihada za kuhakikisha chama inamiliki vyombo vyake vya habari ikiwemo radio ya bahari ili kurahisisha kazi ya Uenezi.
Ameeleza kuwepo kwa vyombo vya habari vya Chama, idara hiyo itasaidiwa kurahisisha utendaji wake wa kazi ikiwemo kusambaza mambo mazuri yanayofanywa na CCM pamoja na Rais Dk.Shein na kwamba imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
 Waride amesema licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji na kisiasa uongozi wake ulijitahidi kuimarisha mazingira mazuri ya kusambaza taarifa na shughuli za Chama ili Wana CCM na wananchi wajue utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020.
Hata hivyo Bi.Waride amemshauri Katibu huyo mpya kuhakikisha anafanya kazi kwa ushirikiano na Watendaji wa ngazi mbali mbali za Chama na Jumuiya zake kwa lengo la kufanikisha kwa ufanisi shughuli za Chama.

No comments