ALI SALUM 'KIROVA'-AZUNGUMZIA UMUHIMU WA MAFUNZO YA ITIKADI
MWAKILISHI wa Jimbo la Kwahani, Mhe Ali Salum Haji akifungua mafunzo ya Darasa la Itikadi katika Tawi la CCM Sebleni. |
VIJANA wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wameshauriwa kujiunga na madarasa ya itikadi ili kunufaika na
fursa mbali mbali zikiwemo kujua historia halisi ya Zanzibar, mwenendo wa
kisiasa, uzalendo pamoja na elimu ya kujitambua.
Ushauri huo
umetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Zanzibar Ali Salum Haji wakati
akifungua mafunzo ya darasa la Itikadi katika Tawi la CCM Sebleni
Zanzibar.
Amesema baadhi ya
vijana wa CCM wanapoteza muda katika vikundi visivyokuwa na faida badala ya
kujiunga na madarasa hayo kwa lengo la kupata elimu juu ya masuala ya
siasa na historia.
Amefafanua kuwa
mafunzo ya itikadi ndio njia mbadala ya kuwakomboa kifikra vijana wa Chama Cha
Mapinduzi ili wawe makada imara wenye misimamo isiyoyumba kisiasa, kiungozi na
kiitikadi.
“ Vijana
someni historia ya nchi yetu kwani kuna mambo mengi yanayopotoshwa na wapinzani
kwa makusudi ili vijana mtoke katika msimamo wenu wa kulinda na kutetea maslahi
ya Chama Cha Mapinduzi.”, amesema Salum.
Kupitia ufunguzi wa
mafunzo hayo Mwakilishi huyo amesisitiza umuhimu wa Wana CCM kuifanyia kazi
falsafa ya siasa na uchumi ili kuwa wabunifu wa kutumia vizuri fursa
zilizowazunguka katika mazingira wanayoishi kwa lengo kujipatia kipato cha
kujikwamua kiuchumi.
Pia ameahidi
kuwalipia mafunzo ya ujasiriamali vijana wote watakaohitimu mafunzo hayo ya
itikadi ili baada ya kupata ujuzi wajiajiri wenyewe.
Naye Katibu wa
Siasa na Uenezi CCM Wilaya ya Mjini, Fatma Haji Mohamed amesema ufunguzi wa
darasa hilo ni miongoni mwa mikakati ya kudumu iliyopangwa na Wilaya hiyo
kupitia mpango kazi wao.
Amesema lengo
la kuanzia mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana na wananchama juu ya
kutambua masuala ya Itikadi na Siasa zinazoendana na zama za sasa katika
ushindani wa kisiasa.
Amesema mpango huo
utakuwa endelevu katika Matawi na Wadi zote za Wilaya hiyo sambamba na
kuwapatia vijana hao elimu ya ujasiria mali.
Jumla ya vijana 76
wameanza mafunzo hayo katika Tawi la Sebleni, na yatachukua muda wa miezi
mitatu.
KATIBU wa Siasa na Uenezi CCM Wilaya ya Mjini, Ndugu Fatma Haji Mohamed akizungumza na vijana na Wana CCM katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Darasa la Itikadi. |
MWALIMU wa Darasa hilo Ndugu Abdallah Juma Nafaika akitoa nasaha zake katika hafla hiyo. |
BAADHI ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa makini nasaha mbali mbali zinazotolewa na viongozi katika hafla hiyo. |
Post a Comment