Header Ads

Vijana, Wanawake kukombolewa na 'UMOJA NI MAENDELEO' Z'BAR



UONGOZI wa Jumuia ya ‘Umoja ni Maendeleo’ ya Kwazani shehia ya Wambaa wilaya ya Mkoani Pemba, imeazimia kuwakomboa vijana na wanawake katika kufikia ndoto zao za maisha, kwa kuwapa elimu ya kilimo, ufugaji na ujasiriamali.

 Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Haji Juma Haji, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari skuli ya Wambaa, juu ya azma na mwelekeo wa Jumuia kwa wanawake na vijana.

Alisema ingawa bado jumuia yao ni change, lakini wanayo mikakati kambambe ya kuhakikisha vijana wa shehia ya Wambaa wananuafaika na kazi za ufugaji, kilimo, ujasiriamali ambapo hayo yatakuja, baada ya kuwapa elimu ya kufikia ndoto zao.
Alieleza kuwa, baada ya kukaa na kuona vijana na hasa wanawake wanakosa fursa za ajira serikalini na hata kwenye hoteli, ndio maana wakaamua kuanzisha Jumuia hiyo, ili kusaka mwarubaini wa tatizo ya kipato, linalowakumba vijana kadhaa kwenye shehia yao.

“Mimi naamini Jumuia hii kama tukishikamana vilivyo sisi viongozi na wanachama wetu, basi miaka michache ijayo, nusu na robo ya wanawane na vijana wa shehia ya Wambaa watakuwa wameshaanza kujitegemea,”alieleza.

Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, alisema katika kufikia lengo lao, amewaomba wale wenye uwezo wa kitaalamu kushirkiana na uongozi wa Jumuia, ili kutimiza malengo yao.
Nae Katibu wa Jumuia hiyo ya Umoja ni Maendeleo Juma Ali Salim, alisema lazima viongozi wajifahamau vyema, kwamba wamebeba jukumu la kuwatafutia njia ya kuondokana na utegemezi vijana na wanawake.

Alisema ijapokuwa wana kazi nyingi za kufanya kwa mujibu wa katiba yao, lakini miongoni mwa vipaumbele vyao, ni kuwapa elimu ya ufugaji, kilimo, uhifadhi wa mazingira, maadili jamii ya shehia ya Wambaa, lakini hawatosahau suala la kukuza elimu hasa wa waliokosa kwenda skuli na mtoto wa kike.

Hata hivyo Katibu huyo, amewaomba wananchi wa shehia ya Wambaa kuendelea kuwaunga mkono kwenye Jumuia yao, ili kusaidiana katika kufikia malengo na dhamira yao.

Nae mjumbe wa kamati tendaji ya Jumuia hiyo, Khamis Mohamed Haji, alisema lazima viongozi waendelee kushikamana kwa karibu, ili hamu ya wanachama ya kuletewa maendeleo.
Baadhi ya wananchi wa shehia ya Wambaa, wamesema hawajamini sana kuwa viongozi hao wanaweza kufikia ndoto za wanawambaa kama walivyoazimia.

Jumuia ya Umoja ni Maendeleo iliopo Kwazani shehia ya Wambaa wilaya ya Mkoani, ambayo imeanzaishwa mwaka jana, inakusudia kulinda mazingira, kuhamasisha suala la elimu, kilimo na ufugaji ambapo ina wanachama 30.

No comments