Rais Dk. Shein: Wahabarisheni wananchi mafanikio yaliyopatikana nchini
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein, amewataka viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuwaeleza wananchi mafanikio makubwa yaliopatikana kutokana na juhudi za
Serikali yao.
Dk. Shein aliyasema hayo wakati akifunga Semina ya Utawala Bora na
Uchumi katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini
Zanzibar, iliyowashirikisha viongozi wa Wizara na Taasisi mbali mbali
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akifunga Semina hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa mafanikio
yaliopatikana ni makubwa sana hivyo ni vyema wananchi wakaelezwa kupitia
vyombo vya habari, wanasiasa na hata viongozi wa Taasisi na Wizara za
Serikali pia, wanapaswa kuwaeleza wananchi mafanikio hayo.
Alieleza kuwa hatua iliyofikiwa ni kubwa sana hivyo ni vyema viongozi
wakawaambia wananchi kwa kila ngazi kuazia Shehia, Wilaya, Mikoa na
Serikali yote kwa ujumla kuwaeleza wananchi jinsi Serikali yao
ilivyopata mafanikio kwani viongozi hao wana haki ya kuongea na wananchi
sehemu yoyote.
“Kuna mambo mengine tunachukua muda mrefu kuwaeleza wananchi hivyo
ni vyema tukatumia mbinu na vyombo vya habari na hata sisi wenyewe
kuwaeleza wananchi mafanikio ya Serikali……kwa vyoyote vile hatua
tuliofikia ni nzuri na tusione tabu kuwaeleza wananchi kwani sisi
tunawajika kwao, ndio waliotuchagua”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa uchumi wa Zanzibar uko
vizuri, hivyo ni lazima ukaendelezwa sambamba na kuthamini kazi kubwa
iliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa viongozi wote kuwa na nakala za
Mipango Mikuu ya Serikali katika ofisi zao pamoja na kutumia nakala za
semina hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi kama ni nyenzo
muhimu katika kutekeleza majukumu yao.
Alieleza matumaini yake kwamba mafunzo ya semina hiyo yatakuwa na
mchango mkubwa katika kujenga kasi na hamasa za utendaji kwa viongozi
hao pamoja na wale walio chini ya dhamana zao.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa kasi iliyofikiwa
katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar tokea mwaka 2010 hadi hivi leo ni
kubwa hivyo ni vyema ikaendelezwa na wananchi wakaelezwa.
Alieleza kuwa viongozi wote wanawajibika kwa wananchi hivyo ni vyema
wakajua kuwa wananchi wanamataraji makubwa kutoka kwao na si vyema
wananchi wakalalamika hatua ambayo inatokana na kutojua na kutoelezwa
mafanikio yaliofikiwa na Serikali yao.
Nae, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib
ambaye pia, ni Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango akitoa neno la shukurani
kwa Rais Dk. Shein, alimpongeza kwa ushiriki wake katika Semina hiyo ya
siku moja ambapo Dk. Shein ndiye aliekuwa Mwenyekiti wa Semina hiyo.
Waziri Salama alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake kubwa za
kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, Waziri huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa kila kiongozi
aliyeshiriki katika semina hiyo atalitekeleza agizo lake la kuyafanyia
kazi mafunzo waliyoyapata ikiwa ni pamoja na kwenda kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili chama hicho kiendeleze
ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
Akitoa mada juu ya “Mwenendo wa Uchumi wa Zanzibar Kuelekea Mwaka
2020”, Dk. Rahma Salum Mahfoudh alieleza kuwa katika kipindi hichi cha
uongozi wa Serikali ya Awamu ya Saba Zanzibar imepata mandeleo makubwa
katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ambayo ni matokeo ya
utekelezaji mzuri wa Dira ya Maendeleo, MKUZA na Ilani ya Uchaguzi ya
CCM.
Aliwasisitiza viongozi wote wa Serikali kwa kutumia dhamana zao
walizopewa kuendelea na kasi hiyo na kuimarisha mashirikiano ili kufikia
malengo yaliopangwa katika Mipango ya Maendeleo ambayo mingi ya Mipango
hiyo inamalizika katika kipindi cha mwaka 2020.
Hata hivyo, alisisitiza haja ya kutumia uzoefu uliopatikana katika
utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo katika kipindi kilichopita ili
kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza
katika kipindi hiki kiliopo.
Nao viongozi hao wakichangia mada saba zilizotolewa katika Semina
hiyo, walieleza mafanikio ya kiuchumi yaliopatikana hapa Zanzibar na
kusisitiza haja ya kuendelezwa ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.
Sambamba na hayo, viongozi hao walieleza kuwa siri kubwa ya mafanikio
hayo ni kuwepo kwa mashirikiano pamoja na amani na utulivu hapa
Zanzibar na kusisitiza kuwa hawatokuwa tayari kuwaona watu wachache
wakitaka kuivuruga amani iliyopo.
Post a Comment