Balozi Seif aonya Ujenzi kataka Vyanzo vya Maji
MAKAMU
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akizindua mradi wa visima
vya maji vilivyochimbwa na Taasisi ya Zanzibar Relief and Development
Foundation (ZARDEF) chini ya usimamizi wa ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania
katika vijiji vya Donge na Mahonda.
|
MAKAMU wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amehimiza wananchi kuacha kuharibu mazingira na
kujenga katika vianzio vya maji, kwani kunachangia upungufu wa huduma hiyo.
Alieleza hayo katika hafla ya
ufunguzi wa visima vya maji safi na salama katika skuli ya msingi Mahonda na
kituo cha afya Donge Mbiji Mkoa wa Kaskazini Unguja, vilivyofadhiliwa na
taasisi ya ZARDEFO FOUNDATION kupitia ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.
Alisema wapo baadhi ya watu
kwa makusudi wanakata miti ovyo na kuharibu miundombinu ya huduma za kijamii
jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi za serikali na washirika wa maendeleo
katika kutatua changamoto zilizopo.
Alisema ni lazima wananchi
wawe na utamaduni wa kuheshimu na kuitunza miundombinu inayojengwa kwa ajili ya
upatikanaji wa huduma za kijamii, yakiwemo maeneo ya skuli.
Alikiri kwamba wananchi
wanakabiliwa na shida ya maji safi na salama hasa katika mkoa wa
kaskazini Unguja, hivyo ili kuikabili shida hiyo ni vyema jamii kuvilinda
vianzio vya maji.
Aliahidi serikali itayafanyia
kazi maombi ya taasisi hiyo ikiwemo kutoa ushirikiano katika miradi ya kilimo
cha mboga na uvuvi, inayotarajia kuianzisha.
“Ajira sio kufanya kazi
serikalini pekee badala yake ni sehemu yoyote ambayo utapata kipato cha
halali, tujitahidi miradi inapokuja tuipokee kwa ajili ya maslahi ya vijana
wetu,” alisema.
Waziri wa Fedha na Mipango,
Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema kutokana na ongezeko la idadi ya watu,
kumeibuka mahitaji makubwa ya maji safi na salama.
Hata hivyo, alisema serikali
inaendeleza juhudi za kuimarisha miundombinu ya maji ili kuwapunguzia shida wananchi
wake.
Post a Comment