CCM Z'bar yawataka Wananchi kufuata maelekezo ya SMZ kujikinga na Maafa
NYUMBA ya Farid Issa iliyoezuliwa na upepo na mvua katika shehiab ya Pwani mchangani. |
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewataka wananchi
kufuata maelekezo na ushauri wa Serikali juu ya kujikinga na maafa yanayotokana
na mvua za masika.
SHEHA wa shehia ya sebleni Khalfan Salum(wa kwanza kushoto) akitoa maelezo ya athari za nyumba zilizopata maafa katika eneo la shehia ya Kwa wazee. |
Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Idara ya
Organazesheni CCM Zanzibar Bakar Hamad Khamis, alipotembelea maeneo mbali mbali
yaliyoathiriwa na mvua katika Mikoa ya Mjini na Kaskazini Unguja.
Alisema kila mwananchi anatakiwa kuchukua
tahadhari kwa kufuata maelekezo ya Serikali hasa kuepuka kujenga katika
maeneo hatarishi kwa lengo la kujikinga na madhara hayo yanayosababishwa na
mvua za masika zinazonyesha kila mwaka nchini.
KATIBU wa NEC, Idara ya organazesheni Bakari Hamad Khamis akionyeshwa nyumba za shehia ya sebleni zilizoathiriwa na mvua. |
Bakari alisema lengo la ziara hiyo ni kuwafariji
wananchi wote waliopata majanga sambamba na kuitaka serikali kupitia mfuko wa
maafa iharakishe misaada kwa wananchi ambao nyumba zao zimebomolewa na mvua
hizo.
Akizungumza Katibu wa Wilaya ya Mjini Fatma
Shomari, alisema katika Wilaya hiyo jumla ya nyumba 68 zimeathiriwa na mvua
hizo pamoja na kusababisha kifo cha mtoto Ramadhan Juma Khamis (4) katika
shehiya ya Sebleni.
“Bado tunaendelea kukusanya taarifa za wananchi
mbali mbali waliopata maafa katika Wilaya yetu ili tuziwasilishe kwa serikali
kwa ajili ya hatua stahiki za misaada”, alisema Katibu huyo.
NYUMBA zilizoingiliwa na maji katika shehia ya Kwa wazee Wilaya ya Mjini Unguja. |
Kwa upande wake sheha wa shehia ya Kwa wazee
Khalfan Salum alieleza kuwa jumla ya nyumba 130 zenye wakaazi wanaokisiwa
kufikia 1300 zimeathiriwa na mvua hizo na wananchi wa maeneo hayo wamehama na
kutafuta hifadhi kwa majirani waliopo katika maeneo salama.
Akizungumza mkaazi wa eneo hilo Haji Makame
‘London’ aliiomba serikali kupitia Manispaa ya mjini kuharakisha mradi wa
ujenzi wa mtaro mkubwa utakaokuwa ukisafirisha maji yanayotwaama katika maeneo
hayo ambayo kwa sasa ni makaazi ya kudumu kwa wananchi.
Aidha Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja,
Mulla Othaman Zubeir alisema zaidi ya nyumba 18 na boti sita za uvuvi aina ya
mtando na ngwanda zimeharibiwa na mvua zilizonyesha katika maeneo mbali mbali
ya mkoa huo na kuathiri mali za wananchi.
Mbali na maafa hayo Mulla alifafanua kuwa maafa
hayo yamesababisha kifo cha mtoto wa mwaka mmoja aliyetumbukia katika shimo la
takataka katika shehia ya Chaani kubwa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Akiwafariji wananchi wa Mkoa huo Katibu wa NEC,
Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakari Hamad aliuagiza uongozi wa CCM Mkoa
huo kusaidia shughuli za ujenzi wa nyumba ya Mkaazi wa shehia ya Mwange Mbaki
Makame Ali (54), ambaye nyumba yake imeanguka kutokana na mvua zinazonyesha
nchini.
Katibu huo wa Organazesheni Bakari aliwasihi
wananchi waliopata maafa kuwa wavumilivu kwa kipindi hichi, huku Chama Cha
Mapinduzi kikiendelea kuisimamia serikali iharakishe misaada kwa wananchi
waliopata maafa hayo.
Naye mkaazi wa shehia ya Mkwajuni
Kero Chumu Juma alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuendeleza utamaduni
wa waasisi wa ASP waliokuwa wakiwatembelea wananchi mara kwa mara kwa lengo la
kuratibu changamoto zao na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali.
“Nimefurahi sana kuona uongozi wa CCM umekuja
kunifariji kwani utamaduni huu ulikuwa umepotea kwa muda mrefu na kwa sasa
naona umerudi kwa kasi kubwa, hii inaonyesha wazi kuwa Chama kinarudi kwa
wananchi wake”, alisema Mkaazi huyo ambaye ukuta wa nyumba yake ulianguka
kutokana na mvua hizo.
Maeneo yaliyotembelewa katika ziara hiyo ni
shehia ya Sebleni, Kwa wazee, eneo la Mtumwa jeni, Pwani mchangani, Chaani
kubwa, shehia ya Kibeni, Shehia ya Mwange, shehia ya Mkwajuni na Mwanga pwani.
Post a Comment