Header Ads

' Wadau jitokezeni kukuza Vipaji vya Wanamichezo Zanzibar'


Image result for vipaji vya wanamichezo 
Makampuni na mashirika binafsi yametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali ya Zanzibar katika kukuza vipaji vya wanamichezo kwa kudhamini michezo mbali mbali ili kuleta maendeleo ya jamii.

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud ametoa wito huo alipokuwa akizindua mashindano ya umoja wa shule za sekondari Tanzania kanda ya Zanzibar katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar ulioambatana na ugawaji wa vifaa vya michezo vilivyotolewa na kampuni ya Cocacola.

Alisema serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar imeanzisha mpango wa kukuza michezo katika skuli 55 unatambulika kama ‘Sports 55’ uliolenga kuibua na kuviendeleza vipaji vya wanafunzi wanamichezo ili kutoa matokeo bora kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Alisema katika utekelezaji wa mpango huo serikali imejidhatiti kuzalisha walimu, waamuzi, upatikanaji wa vifaa vya michezo na  kujenga viwanja katika kila wilaya kitakachoweza kutumiwa kwa ajili ya michezo zaidi ya mmoja.

“Toka ameingia madarakani Rais wa Zanzibar amekuwa akihimiza uwepo wa vuguvugu la michezo ili kuirudishia nchi yetu (Zanzibar) hadhi yake katika medani ya michezo jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono na kila mmoja wetu katika nafasi aliyopo”, alisema Mahmoud.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza kampuni ya Cocacola kwa kuamua kudhamini mashindano ya UMMISETA kwa mwaka wa 3 mfululizo na kuwaasa walimu na wanafunzi kuvitunza vifaa vilivyotolewa ili viweze kutumika kwa muda mrefu.

“Mnapofanya hivi sio tu mnasaidia juhudi za serikali katika kuimarisha michezo nchini bali pia mnajikaribisha kwa jamii kwani hiki mnachokuifanya ni sehemu ya kurudisha faida mnayoipata kwao kitu ambacho kinapaswa kuzingatiwa na taasisi nyengine”, alieleza Mahmoud.

Nae Mkurugenzi wa mawasiliano na matukio kijamii wa kampuni ya Coca cola Haji Mzee Ally alisema kampuni yake imeamua kudhamini mashindano hayo ili kusaidia upatikanaji wa viwango bora na wachezaji katika michezo mbali mbali na kkwamba kampuni hiyo itaendelea kufanya hivyo katika siku za usoni kutokana na kuonesha kuleta matokeo chanya.

“Tulipoanza kudhamini haya miaka miwili iliyopita tulilenga kuleta hamasa na mabadiliko katika sekta ya michezo kitu ambacho tumefanikiwa nacho kwa kiasi kikubwa”, alisema Haji.

Awali akitoa taarifa katika tukio hilo, Mkurugenzi wa kamisheni ya michezo na utamaduni wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Hassan Tawakal Khayrallah alisema skuli 20 zitapatiwa jezi, viatu na mipira kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya kanda kabla ili kupata timu zitakazoshirikia mashindano ya UMISETA taifa yatakayofanyika baadae mwaka huu mjini Mwanza.


No comments