Shamata: Tunajenga haya Matawi kuimarisha CCM yetu
![]() |
MWAKILISHI
wa jimbo la Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Shamata Shaame Khamis amewahakikishia wanachama wa
Chama cha Mapinduzi –CCM- kuendelea kushirikiana na viongozi mbalimbali wa
matawi katika utekelezaji wa majukumu ya Chama ikiwemo upatikanaji wa Ofisi za
Chama katika kila Tawi jimboni kwake.
Kauli
hiyo ameitoa wakati akizungumza na vijana mara baada ya kukamilika kwa zoezi la
uwekaji wa kifusi katika Ofisi ya CCM Tawi la Maziwang’ombe inayojengwa kupitia
juhudi za mwakilishi huyo.
![]() |
Mwakilishi wa jimbo
la Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Shamata Shaame Khamis akishiriki
zoezi la utoaji wa Kifusi katika Jengo la Ofisi ya CCM Tawi la Maziwang’ombe.
|
Khamis
amesema kuwa, lengo la ujenzi wa ofisi za CCM katika Matawi yake ni kuhakikisha
inaendelea kuwatumikia wananchi kwa ukaribu, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi
ya wanachama zaidi.
“lengo la kutengeneza matawi si kwamba chama
kinakuwa kinatengeneza fedha, bali kazi yake kubwa ni kuhakikisha CCM
inaendelea kushinda katika chaguzi mbalimbali na huu ndio mtaji wetu,” alisema
Mwakilishi huyo.
Katika
hatua nyingine mwakilishi huyo aliendelea kuwasisitiza vijana kujiepusha na
vitendo vya utumiaji wa Dawa za kulevya kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
haipo tayari kuona vitendo kama hivyo vinaendelea kujitokeza ndani ya wilaya
hiyo.
“Tunaona
juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Uongozi wa Wilaya yetu chini ya Mkuu
wa Wilaya, Salama Mbarouk Khatib wa kupambana na Dawa za kulevya pamoja na
Pombe haramu, hivyo basi nakuombeni sana jiepusheni kujiingiza katika masuala
haya kwani endapo utagundulika hatua kali zitachukuliwa dhidi yako,” alisema
Shamata.
![]() |
Katibu wa Tawi,
Khatib Said Juma akimwelezea Mwakilishi Shamata kuhusu ujenzi wa Afisi za Tawi
hilo
|
Katibu
wa Tawi hilo, Khatib Said Juma amewapongeza vijana kwa kuendelea kuwa na moyo
wa kujitolea na kuwataka kuendelea kutoa mashirikiano kwa viongozi wao ili
kuona kwamba maendeleo yanapatikana kwa haraka zaidi.
“Niwashukuruni
sana vijana kwa kazi mliyoifanya leo, na nawaombeni muendeleze mashirikiano haya
baina ya viongozi wetu wa Chama na Serikali ikiwa ni pamoja na kuendelea
kudumisha Amani katika maeneo yetu,” alisema Juma.
Awali Mwenyekiti wa UVCCM wa Tawi hilo, Juma
Mbarouk Khamis, akimkaribisha Mwakilishi huyo katika Zoezi hilo, alimuahidi
Mwakilishi kwamba Vijana wa Tawi la Maziwang’ombe wataendelea na juhudi zao za
kukitumikia pamoja na kukilinda Chama hicho ili kiendelee kuaminika zaidi kwa
wananchi wake.
“Ndugu
Mheshimiwa, naomba tukuhakikishie tu kwamba, sisi vijana wa Tawi hili la
Maziwang’ombe tupo tayari kuendelea kutoa nguvu zetu kwa vyovyote vile ili kuhakikisha
CCM inaendelea kuaminika kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuendelea kushinda
katika chaguzi zote, na ndiomana tumeamua kuungana pamoja hapa kuhakikisha
tunafanikiwa ujenzi wa Tawi hili,” alisema Mwenyekiti huyo.
Ujenzi
wa Jengo la Ofisi ya Tawi la CCM katika Wadi ya Kiuyu-Maziwang’ombe Wilaya ya
Micheweni, ni moja ya juhudi za Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Shamata Shaame
Khamis, za kutaka kuimarisha nguvu za Matawi kwa kuwa na Ofisi zake, ambapo jengo
hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2018.
Post a Comment