Header Ads

Kikao Baraza la Madiwani Micheweni: Mbinu Mpya Usimamizi wa Mapato zatolewa, DC Salama kama kawaida 'atema cheche'

MADIWANI katika Halimashauri ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametakiwa kuwa makini katika usimamizi wa miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Majimbo ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya wananchi wao.

Akizungumza katika Kikao cha kujadili ripoti ya mapato na matumizi kwa robo ya tatu ya mwaka, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa halimashauri hiyo, Omar Issa Kombo amesema ili Serikali iweze kutekeleza malengo yake ni lazima viongozi wawe mfano wa kuigwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa halimashauri ya Wilaya ya Micheweni, Omar Issa Kombo akifungua kikao cha Kujadili Ripoti ya Mapato na Matumizi ya Robo  Mwaka wakati wa kikako hicho
Amesema kuna miradi mbalimbali ya Jimbo ambayo inakuwa inaelekezwa kwa wananchi ambayo hughalimu kiasi kikubwa cha fedha, hivyo madiwani wanatakiwa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa bila ubadhilifu wa aina yoyote.
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Salama Mbarouk Khatib (kulia) akipitia Ripoti ya  Mapato na Matumizi ya Robo  Mwaka wakati wa kikako hicho cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni
Mkuu wa Wilaya hiyo Salama Mbarouk Khaatib akichangia katika kikao hicho amewataka madiwani kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato, ikiwa ni pamoja baraza kuepukana na utitili wa miradi na badalayake waandae vipaumbele katika utekelezaji wa miradi hiyo.

"Niwajibu wetu kuhakikisha tunaziba mianya, kwa sababu hiki ambacho kinakusanywa ndicho ambacho kinategemewa kujengwa kwa wananchi kwani wananchi wana mahitaji mengi, hivyo bila ya sisi kujipanga tutashindwa kukamilisha mahitaji ya wananchi wetu," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha katika hatua nyingine mkuu huyo wa Wilaya amewataka madiwani kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Wilaya katika vita ya kupambana dhidi ya Madawa ya kulevya.

"Mapambano dhidi ya Dawa za kulevya hayana Siasa, Dini, Jinsia wala Ukabila hili pia limekuwa nii gumzo sana kwa Wilaya hii, sasa Micheweni akikamatwa mtu utasikia huyo CCM, sasa wale ambao suala hili mnaliangalia kwa mitazamo yenu kwangu halina nafasi, mimi nitaendelea kusimamia wajibu wangu na kama mkiona sifai pendekezeni mseme mimi naondoka kwa sababu  ya kupambana dhidi ya Dawa za kulevya mimi nipo tayari," alisema.

Katika robo ya tatu ya kuanzia mwezi januari mpaka machi mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 64, 365000 huku zaidi ya shilingi 45 milioni, zikiwa zimetumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

(PICHA ZOTE NA GASPARY CHARLES- Micheweni Redio

No comments