Header Ads

Miaka 46 Kumbukumbu ya Mzee Karume


WAZANZIBARI  wamo katika kumbukumbu muhimu sana ya kutimia miaka 46 tangu rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu mzee Abeid Amani Karume alipofariki dunia.

Kwa hakika hilo ni tukio muhimu sana katika maisha ya Wazanzibari, kwani wanakumbuka mazuri mengi ya kupigiwa mfano aliyoyafanya hayati Karume enzi za uhai wake, likiwemo tukio kubwa kabisa la kuleta Mapinduzi ya Zanzibar, baada ya kutawaliwa kwa muda mrefu na wakoloni.

Ni dhahiri kuwa unapotaka kuzungumza mambo ambayo yanamgusa mzee Karume  unaweza kuandika kurasa nyingi zaidi, na pengine usifikie mwisho wake kutokana na mambo mengi na mazuri aliyoyafanya.

Mzee Karume unaweza kumzungumzia mazuri yake katika nyanja mbali mbali ikiwemo kilimo, elimu, utamaduni, michezo, siasa na mengine mengi, ambayo yote hayo hadi leo kila mmoja anaona matunda yake.

Katika makala hii licha ya mengi ambayo mzee Karume aliyafanya nitazungumzia japo kwa ufupi baadhi ya miundombinu ya viwanja vya michezo ambavyo mzee Karume aliviweka, ambavyo hadi leo bado vinaendelea kutumika kwa faida ya Wazanzibari na kuleta manufaa makubwa kwao kimichezo.

Mpira wa miguu ni miongoni mwa michezo inayopendwa na watu wengi duniani, pengine kulinganisha na michezo mingine ambayo nayo pia hupendwa kulingana na nchi zao, lakini kwa soka umekamata namba moja.

Historia inaonesha kuwa soka lilianza kupendwa tangu miaka ya nyuma kabla na baada ya Mapinduzi, hivyo ni wazi kuwa mchezo wa soka una historia kubwa sana Zanzibar.

Lakini baada ya Mapinduzi mwaka 1964, Serikali ya Zanzibar ilichukuwa juhudi mbali mbali za kuuimarisha zaidi  mchezo huo, na kufikia hatua ya kujengwa kwa uwanja wa Amaan.

Hatua hiyo ya kujengwa uwanja wa huo ilikuwa nia njema kabisa ya kuwa na uwanja wa kisasa, ambayo  ilikuwepo siku nyingi tangu ilipopatikana serikali ya wananchi wa Zanzibar.

Kwa hakika kila mmoja anafahamu umuhimu wa kuwa na viwanja vizuri vya michezo sio tu enzi hizo hata leo, ambapo nchi zilizoendelea zimekuwa na viwanja bora kabisa,  nia ambayo alikuwa nayo mzee Karume.

Kutokana na muono wa mbali kabisa ambao mzee Karume alikuwa nao, aliamua kuanza harakati za kujenga kiwanja cha michezo cha kisasa na cha kimataifa ili wananchi wake wapate fursa nzuri ya kushiriki michezo hasa mpira wa miguu.

Kuanzia Septemba 17, 1967 Rais wa Kwanza  wa ASP,Mzee Abeid Amani Karume,alianza mbio za ujenzi wa uwanja wa Amaan, baada ya kuwakusanya na kuwaongoza wananchi kufyeka mahali  palipokusudiwa kujengwa  uwanja huo huko Sebleni.

Katika kuona jambo hilo linafanikiwa wazee kwa vijana,wanaume kwa wanawake,wakuu wa chama na serikali  pamoja na wananchi walishiriki vilivyo katika ufyekaji huo.

Wananchi hao bila ya kujali vyama vyao, mvua wala jua walijumuika pamoja katika kusafisha eneo hilo ambalo limetumika kwa ujenzi wa uwanja wa Amaan, na hadi sasa si haba wananchi wa visiwa hivi wananeemeka na uwanja huo.

Eneo la ekari 22  lilipatikana mapema kuliko ilivyotarajiwa ambapo wananchi mbali mbali wakiongozwa na marehemu mzee Abeid Karume walianza matayarisho ya uwanja.

Mnamo Novemba 1969,ujenzi wa kiwanja ulipamba moto pamoja  na  Januari 12 , 1970, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ,aliufungua uwanja huo uliopewa jina la ‘AMAAN’.

Mara baada ya kumalizika kujengwa uwanja huo  pambano la kwanza lilifanyika baina ya timu ya Young African na timu mchanganyiko ya Elimu na Wanamaji wa Zanzibar, mchezo huo ulikuwa mkali na kusisimua ambapo timu hizo zilitoka sare.

Ujenzi wa uwanja huo wa kisasa pamoja na hoteli ya uwanja wa kwa ujumla wake ikiwemo  vifaa vyake vyote viligharimu shilingi  6,000,000 za kitanzania.

Lakini  uwanja huo mkubwa ambao umetimia vipimo vyote, pia pembezoni mwa uwanja huo  vipo viwanja vidogo vidogo kwa ajili ya mazoezi, lakini hivi sasa pia vinatumika kuchezewa mechi za madaraja mbali mbali ikiwemo pia vijana.

Kwa hakika ni faraja kubwa sana kwa wananchi wa Zanzibar kuwa na kiwanja hiki cha kisasa, ambacho hadi leo  kinaendelea kuwa kiwanja kikubwa na chenye hadhi ya kimataifa, ambapo michezo mbali mbali ya kimataifa huchezwa.

Mbali na kiwanja hicho cha zamani ambacho marehemu Karume alikisimamia kwa nguvu zote, pia kiwanja cha Gombani pia ni miongoni mwa viwanja ambavyo vipo Zanzibar na hadi leo vinatumika katika michezo ya Kimataifa.

Mbali na uwanja huo wa Amaan pia Zanzibar ilipata nafasi nyingi muhimu ya kuwa na uwanja wa mpira wa miguu wa Mao Dzedong, amabo nao umeleta faraja nyingine kwa wanamichezo baada ya serikali ya China kuamua kujenga uwanja huo.

Uwanja wa Mao Dzedong ambao hivi sasa serikali hii ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya watu wa China, zimeamua kuufanyia matengenezo makubwa ili kuurejeshea hadhi yake, kwani ni moja ya viwanja ambavyo vimebeba historia kubwa sana katika visiwa vya  Zanzibar pamoja na nchi ya China.

Historia inaonyesha kuwa mashindano ya kwanza ya Afrika Mashariki Goseji , ambayo hivi sasa yanajulikana kwa jina la Chalenji yalifanyika kwenye uwanja wa Mao Tse-tung Mwaka 1949, wakati huo uwanja huo ukijulikana kwa jina la ‘Seyyid Khalifa Sports Ground’.

Hata hivyo kutoka mwaka 1947 – 1966 Zanzibar ilikuwa ikishiriki mashindano hayo lakini haikuwahi kupata ushindi, licha ya kucheza kwa kiwango kizuri bahati haikuwa yao.
Mbali na michezo hiyo pia michezo ya raidha ilikuwa ikifanyika ambapo mwaka  1894 , mashindano ya mwanzo ya riadha yalifanyika baina ya Wanamaji wa H.M.S,  ambao walicheza wenyewe kwa wenyewe, mashindano ambayo yalifanyika katika viwanja vya Coopers hivi sasa vinajulikana kwa jina la viwanja vya Maisara.
Kwa wakati huo licha ya kuwa  yalikuwa mashindano makubwa sana na mazuri, lakini zaidi waliokuwa wakishiriki mashindano hayo ni wanafunzi wa skuli mbali mbali pamoja na askari polisi.

Mbali hayo pia michezo mbali mbali ilionekana kuimarika pamoja na viwanja vyake ambapo michezo ya Tenisi, mpira wa Wavu, Golf ilianza kuchezwa kuanzia mwaka 1888, lakini klabu ambazo zaidi zilikuwa zikishiriki ni zile za kikabila na zaidi walikuwa wakitumia viwanja vyao kwenye maoneo mbali mbali.

Mbali na viwanja hivyo vya mpira wa miguu pia vipo viwanja vyengine ambavyo maarufu vinajulikna kwa viwanja vya kufurahishia watoto, ambavyo vipo Tibirinzi Pemba na Kariakoo Unguja.

Mawazo ya kuataka kuyanzishwa ujenzoi wa viwanja hivuyo yalitolewa na Mzee Abedi Karume, kwa nia ya kuwafanya watoto kuweza kusherehekea vyema wakati wa skukuu mbali mbali zinapokuwepo.

Uwanja wa Tibirinzi ulianza kujengwa mwaka 1972 wakati huo mzee Karume ameshafariki dunia,lakini  hatua za waloi za ujenzi huo zilianza kwa mzee Karume, ambapo viwanja hivyo viliwekewa pembea za kisasa na kuwafanya watoto kusherehekea kwa amani na furaha tele.
 Chanzo: ZANZIBARLEO

No comments