Tumuezi Mzee Karume kivitendo
SEKUNDE hutengeneza
dakika, dakika hutengeneza saa, saa hutengeneza siku, siku hutengeneza wiki,
wiki hutengeneza mwezi, mwezi hutengeneza mwaka, kwa hakika hivyo ndivyo muda
unavyosonga mbele na maisha kupotea.
Hivi
ninavyozungumza miaka 46 imekatika tangu Zanzibar, wazanzibari na watanzania
kwa ujumla kumpoteza jemedari wa mapinduzi ya Zanzibar ya 12 Januari
1964, marehemu sheikh Abeid Amani Karume.
Haikuwa
rahisi kwa wananchi wengi kuamini kuwa Karume amekufa kutokana na mazingira ya
kifo cha baba yetu Karume, hata hivyo ukweli ulidhibiti kuwa kila kilichoumbwa
kitakufa nae ahadi yake ikawa imefika.
Wananchi
wengi waliangua vilio siku ya mazishi yake, wengine walibakiwa na simanzi kwa
muda mrefu, huku nchi ikiwa kimya kutafakari nini kitatokea Zanzibar ikiwa bila
ya Karume.
Niwaite
bila ya kupepesa macho ama kuwaonea haya kuwa waliopanga na kutekeleza mauaji
hayo ni wahaini, mahasidi, mafataani na wapinga maendeleo ya Zanzibar na
wazanzibari kwa ujumla.
Huku
tukiadhimisha kifo cha Mzee Karume kwa kutimia miaka 46, tunapaswa kutafakari
na kujiuliza mengi, ikiwemo suala kubwa, kweli tumeweza kuzitekeleza ndoto
alizokuwanazo na kutuachilia mzee Karume?
Tunapaswa
tulifikiri hili kwa sababu siku ya mazishi yake zilitolewa hotuba nyingi na
maelezo mengi, lakini kilichovutia kwenye hotuba zote hizo ile semi moja ya
kujipa matumaini.
Semi
hiyo ilieleza hivi, “Mzee Karume ameondoka, kilichoondoka ni kiwiliwili chake,
lakini fikra na mawazo yake yatadumu milele na milele”.
Nadhani
umefika wakati tumfuate Karume kwa vitendo isiwe kwa kauli tu kutoka midomoni
mwetu kwa kuvutiwa na maslahi binafsi.
Ninavyomkumbuka
Karume, hakuwa mbinafsi, hakuwa mpenda makuu, alikuwa akishirikiana na watu,
aliwapenda watu, aliwajali wazee, watoto na jamii yote.
Karume
alisisitiza amani, alikataza utengano, alipinga ubaguzi hasa ukabila miongoni
mwa jamii, kwa sababu alijua ukabila una athari kubwa katika mbio za kuleta
maendeleo.
Alitamani
kila kilichomo kwenye ardhi ya Zanzibar kiishi vizuri na kwa amani, pasi na
kubughudhiwa, kunyanyaswa wala kubaguliwa kwa hali yoyote ile ya kimaumbile
wala kisaikolojia.
Akiwa
katika uongozi wake wa miaka saba tangu mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964
ni wazi kuwa ameacha mambo mengi ya maendeleo ambayo hadi sasa yanaonekana kwa
macho na kuendelezwa zaidi kwa ustawi wa wazanzibari.
Tunakumbuka
huduma bure alizowapatia wananchi kama elimu, afya bure, huduma za maji safi
bure, alitandika miondombinu hasa barabara.
Kubwa
zaidi namkumbuka mzee Karume kwa kutuletea mapinduzi ambayo yametuletea uhuru
wa kujitawala na kujiamulia mambo yetu kama Wazanzibari.
Hivi karibuni
akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein
alisema kuwa mzee Karume ana heshima ya kipekee wazanzibar na watanzania kwa
ujumla.
Ambapo Dk. Shein
alisema juhudi za marehemu Mzee Karume na marehemu Julius Kambarage Nyerere kuziunganisha
Tanganyika na Zanzibar mnamo Aprili 26 mwaka 1964 na hadi hivi sasa muungano
huo umeweza kujijengea sifa kubwa.
Kilichobakia
ni kuyafuata aliyoyasema, kutekeleza ahadi zake na kuyaendeleza aliyoyaacha.
Iwapo haya yote yatazingatiwa kwa kutekelezwa, hakuna sababu ya kumsahau na
kumwombea dua njema shujaa wetu wa Mapinduzi.
Mzee
Karume ameondoka, lakini kilichoondoka ni kiwiliwili chake fikra na mawazo yake
yatadumu milele na milele. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.
Amin.
Post a Comment