Rais Shein atuma Pongezi kwa Mshindi wa Uchaguzi Misri
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za
pongezi Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi kwa ushindi mkubwa alioupata kufuatia uchaguzi Mkuu wa
nchi hiyo uliofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 March mwaka huu.
Katika
salamu hizo, Rais Dk. Shein alimpongeza Rais Abdel Fattah El- Sisi kwa ushindi
wake mkubwa wa kura milioni 21 sawa na
asilimia 97.08 ya kura zote na hivyo kupata ridhaa ya kuongoza tena nchi hiyo
kwa muhula wa pili, ushindi ambao umeonesha wananchi wa Misri jinsi walivyofarajika
na uongozi wa Rais El-Sisi.
Salamu
hizo zilieleza kuwa wananchi wa Misri wameweza kuishuhudia nchi yao ikiendelea
kupata maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Rais El-Sisi katika kipindi chake
cha kwanza cha uongozi wake baada ya kuingia madarani mnamo mwaka 2014.
Aidha, Dk.
Shein alieleza katika salamu hizo kuwa ushindi wake huo mkubwa itakuwa ni njia
moja wapo muhimu ya kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria
uliopo kati ya Zanzibar na Misri.
Rais Dk.
Shein alimuhakikishia Rais Abdel Fattah El-Sisi kuwa Zanzibar itaendeleza
uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Misri sambamba na kuimarisha
udugu uliopo kati ya wananchi wa pande mbili hizo.
Pia, Rais
Dk. Shein alimtakia uongozi mwema kiongozi huyo pamoja na kuendeleza maendeleo
endelevu yaliopatikana nchini mwake huku akimtakia afya njema sambamba na
kuendelea kuimarisha amani na utulivu nchini humo kwa manufaa ya nchi hiyo na
wananchi wake.
Rais Abdel
Fattah El-Sisi mwenye umri wa miaka 63 alichaguliwa tena kuwa Rais wa Misri baada
ya kuibuka na ushindi huo mkubwa ambapo alimshinda mpinzani wake Moussa
Mustapha Moussa kutoka chama cha upinzani cha El Ghad ambaye baada ya matokeo
hayo mpinzani wake huyo alieleza jinsi alivyoridhishwa na matokeo ya uchaguzi
na hatimae alimpongeza Rais El-Sisi kwa ushindi wake huo mkubwa.
Post a Comment