RC KAS PEMBA AKUNWA NA MWENENDO WA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WILAYA YA MICHEWENI
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini
Pemba Mhe. Omar Khamis Othman ameipongeza kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya
ya Micheweni inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Salama Mbarouk Khatib kwa
kufuata maagizo aliyoyatoa ya kupambana na Madawa ya kulevya na pombe haramu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii amesema kuwa kamati hiyo inafanya kazi kwa
mujibu wa matakwa ya Serikali ilivyo agiza.
Mkuu huyo wa mkoa
amesema licha ya juhudi ambazo zinaendelea kuchukuliwa na kamati hizo za wilaya
lakini bado kuna baadhi ya viongozi wanarejesha nyuma utekelezaji wa zoezi
hilo.
“Tumepata taarifa
kuwa kuna baadhi ya viongozi wa serikali ambao bado hawaungi mkono juhudi hizi,
lakini niwahakikishie tu kwamba serikali haitakuwa tayari kumvumilia mtu ambae
ataonekana kwenda kinyume na matakwa ya serikali,” alisema Othuman.
Mapema akithibitisha
taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya katika wilaya ya
Micheweni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Haji Khamis Haji, alisema katika
oparesheni hiyo vijana watatu walibainika wakiwa na Dawa za kulevya aina ya
Bangi.
“Katika Oparesheni iliyofanyika
April 2, na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Micheweni Shehia ya
Makangale, ilifanikiwa kuwakamata vijana hao watatu wakiwa na dawa za kulevya
aina ya Bangi Nyongo nne,” alisema Kamanda huyo.
Akiwataja
watuhumiwa hao kamanda Haji alisema kuwa watuhumiwa waliokamatwa ni Hamis Haji
Ali 37, aliyekamatwa na Nyongo Mbili za Bangi, Miraji Salim Nassor 23 Nyongo
moja na Faki Ali Rashid 20 nyongo moja wote wakazi wa Makangale.
Nae Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya hiyo Bi Salama Mbarouk Khatib, alisema
katika oparesheni hiyo wamejipanga kuhakikisha kwamba Wilaya ya Micheweni haiwi
genge la kuingiza madawa ya kulevya.
“Kamati ya Ulinzi
na usalama wilaya ya Micheweni tumejipanga kuhakikisha tunatokomeza aina yoyote
ya vitendo vya uhalifu ikiwemo kupambana na madawa ya kulevya na Pombe haramu
ili kuwafanya wananchi wetu wajihusishe na shughuli halali za maendeleo,”
alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Oparesheni ya
kutokomeza madawa ya kulevya na pombe haramu inaendelea katika wilaya ya
Micheweni ikiwa chini ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Post a Comment