Header Ads

'Wakulima Fuatilieni Taarifa za Utabiri wa Hali ya Hewa'- TMA

Related image 
MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA)  imewataka wakulima kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na mamlaka hiyo  ili waweze kuzitumia kuchagua mazao ambayo yanayoendana na wastani wa mvua na
hivyo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi .

Mtabiri wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya hali ya hewa nchini Mathew Ndaki amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikitoa taarifa na tahadhari za hali
ya hewa pamoja na kutoa ushauri kwa wakulima kupanda mazao
yanayoendana na wastani wa mvua kwa msimu husika.

Akizungumza na wakulima , wafugaji na wavuvi kisiwani Pemba Ndaki amesema ili kilimo kiwe stahamilivu kwa mabadiliko ya tabianchi ,ni vyema wakulima kuelewa  wastani wa muda mrefu na mfupi wa mvua katika maeneo yao.

“Upatapo utabiri wa hali ya hewa wa msimu panga kilimo chako kwa mujibu wa ushauri uliotolewa kwenye utabiri  na wataalamu  katika eneo
lako ”alisisitiza.

Aidha Ndaki ametaja sababu za mabadiliko ya Tabinchi kuwa ni binadamu wenyewe ambao wamekuwa akiharibu mazingira kutokana na shughuli za uchumi  , ambao wanafanya hivyo bila ya kuzingatia athari za baadaye.

Naye Afisa Kilimo kutoka shirika la Chakula Duniani (FAO) Diomedes Kalisa amesema uhaba wa chakula , mafuriko pamoja na njaa kubwa
zimeweza kuepukika iwapo tu walkuma watakuwa tayari kulima mazao yanayostahamili ukame.

Ameeleza kwamba FAO kwa kushirikiana na mashirika menegine ya kimaendeleo , kupitia ufadhili wa Marekani limeanzisha mradi wa kuwahamaisha wananchi kufuata ushauri wa kitaalamu ili kukabiliana na upungufu wa chakula.

Akichangia kwenye kikao hicho , Afisa Misitu Wilaya ya Micheweni Massoud Suleiman Hamad amesema suala la ukataji miti ovyo unaofanywa na baadhi ya wananchi kwa kisingizo cha shughuli za kiuchumi umesababisha upungufu wa mvua kwa baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.

Massoud ameiomba Mamlaka hiyo kuandaa utaratibu wa kuwafikishia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili waweze kuifikisha kwa wananchi kwa wakati ili kuweza kudhibiti vitendo vya uchafuzi wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ovyo.

Hata hivyo akitoa ufafanuzi juu ya ombi hilo Mecklina Merchades Mtabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa amesema wameanzisha utaratibu wa kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa kupitia simu za mikononi.

Hivyo amewatoa hofu wakulima , wafugaji na wavuvi kwamba wajiandae kupokea taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzifanyia kazi kupitia
simu zao za mikononi wakati wa mvua hizi za masika zinazoendelea kunyesha visiwani hapa.

No comments