Wallace Karia atoa Heshima kwa Vijana wa NGORONGORO HEROES
Ngorongoro
Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Africa
za Vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba baada ya ushindi
wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya
bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini
Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya
mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi.
Rais wa TFF
Ndugu Karia amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa
Tanzania na inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la
vijana.
Amesema
Vijana hao wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na
wanastahili pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi
ya timu hizo.
“Tumepokea
matokeo ya Vijana wetu wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa
kwasababu tumekuwa tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo
yanaonekana uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa
Tanzania kwa ujumla” alisema Karia.
Aidha Rais
wa TFF Ndugu Karia amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi
mazuri zaidi timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali
yanayowakabili.
Amesema
TFF inajivunia vijana hao ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba watu
mbalimbali, taasisi, makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na kuiga mfano wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na kuisaidia Ngorongoro Heroes
katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye mchezo wa marudiano.
Amemalizia
kwa kuwashukuru wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa
Tanzania huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya
Rais John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.
Post a Comment