MBUNGE wa Jimbo la Mahonda, Mhe. Bahati
Ali Abeid amewataka watendaji na viongozi wa ngazi mbali mbali za Chama na
jumuiya katika jimbo hilo kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha taasisi hiyo
kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua
mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo makatibu na wenyeviti wa CCM na
Jumuiya zake ngazi za matawi hadi jimbo huko katika ofisi ya Jimbo la mahonda
iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.
Alisema viongozi hao wanatakiwa kufanya
kazi za CCM na kutekeleza maagizo mbali mbali ya viongozi wa ngazi za juu kwa
lengo la kuongeza kasi ya kuwatumikia wananchi waliokipa ridhaa Chama
kuongoza dola.
Mh. Bahati aliwakumbusha viongozi hao
kwamba wanakiwa kulinda na kutetea maslahi ya CCM kwa kutekeleza majukumu yao
ipasavyo ili Chama kishinde katika uchaguzi mkuu ujao.
alisema viongozi hao wanatakiwa
kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ambayo ni miongoni mwa nyenzo za kurahisisha
majukumu yao ya kiutendaji ndani Chama Cha Mapinduzi.
Alisema baada ya mafunzo hayo
Chama kinatarajia kuona mabadiliko ya haraka ya kiutendaji kutoka kwa viongozi
na watendaji hao.
"Baada ya mafunzo haya mnatakiwa
kusimama imara na kujiamini ili wanachama waliokuchagueni muwe viongozi waone
umuhimu wenu katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.
Pia mnatakiwa kufanya maamuzi na
kujadili matatizo na kero za wanachama kupitia vikao halali vya kikatiba ili
kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima katika ngazi zenu za kiutendaji na
kiuongozi", alisema Mbunge huyo ambaye ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya
Jimbo hilo.
Akitoa mada ya kuliwa kwa CCM, Katibu
wa Kamati maalum ya NEC, Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Bakari Hamad
Khamis, alisema CCM ina historia ndefu ambayo msingi wake unatokana na juhudi
za waasisi wa ASP na TANU ambao ni marehemu Mzee Abeid Amani Karume na
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika kuleta umoja na mshikamano kwa
wananchi.
Alisema mwaka 1964 Chama cha ASP
kiliamua kufanya Mapinduzi kwa lengo la kuwakomboa wananchi wa visiwa vya
Zanzibar, waliotawaliwa kwa mabavu na utawala wa kisultani.
Alieleza kwamba baada ya Mapinduzi hayo
waasisi hao walifanya maamuzi ya kuziunganisha nchi mbili ya Zanzibar na
Tanganyika ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Pamoja na hayo Katibu huyo alifafanua
kuwa mwaka 1977 vyama vya ASP na TANU baada ya kushauriana kwa muda mrefu
vikaamua kuungana na kuunda Chama kimoja chenye nguvu ambacho ni Chama Cha
Mapinduzi(CCM) kwa lengo la kusimamia siasa na demokrasia za kweli kwa wananchi
wa Zanzibar na Tanzania bara.
Katibu huyo Bakari aliwasisitiza vijana
nchini kusoma historia halisi ya Zanzibar ili wajifunze na kutambua mambo ya
maendeleo yaliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake kwa awamu mbali
mbali za uongozi wa dola.
|
Post a Comment