Maoni ya Gazeti la ZANZIBAR Leo kuhusu Sherehe za Mei Mosi
WAFANYAKAZI wa
Zanzibar walioko kwenye sekta rasmi na isiyorasmi, leo wanaungana na wenzao
duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya wafanyakazi maarufu kama ‘May Day’.
Bila shaka hii ni
siku muhimu sana kwa wafanyakazi wa sekta zote kwani wamekuwa muhimili muhimu
katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na hata maendeleo ya ustawi wa
jamii yetu.
Huku
tukiadhimisha siku hii muhimu, ni vyema wafanyakazi katika sekta zote
wakachukua dakika chache kujitathamini kwa kiasi gani wanawajibika kwenye
majukumu yao wanayopaswa kuyatekeleza kila siku.
Suali la
uwajibikaji kwa watumishi na hata baadhi ya viongozi ni gumu mno, na kwamba
pamoja na kusemwa sana wanaoelezwa kama vile wametia pamba masikioni.
Angalau
tunadiriki kusema kwenye sekta isiyo rasmi, walioajiriwa huko wamekuwa makini
kutokana na usimamizi mzuri wa viongozi wao ikilinganishwa na wale wa sekta
rasmi, ingawaje wanatatizo la kudumu ya kupewa mikataba na maslahi madogo.
Wasimamizi wa
majukumu kwenye sekta isiyorasmi wamekuwa wakali kwenye usimamizi wa majukumu,
jambo linalomlazimisha mfanyakazi kuwajibika kwani kinyume chake ni kupoteza
ajira na haki nyengine zote.
Hilo nikinyume
kidogo na sekta ya umma kwani bado suala la kufanyakazi kwa mazoea kwa
watumishi na hata baadhi ya viongozi waliopewa dhamana limekuwa likiendelea,
suala ambalo limekuwa likizorotesha ufanisi kwenye sekta hiyo.
Hatujafanya
utafiti tukajiridhisha, lakini ukweli ni kwamba katika taasisi nyingi za umma
ni nadra sana mtumishi kufanyakazi saa nane anazotakiwa kuwajibika, na ni nadra
sana kumaliza wiki bila ya kuwa na dharura hata kama si ya msingi sana.
Mara kadhaa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein
amekemea kufanyakazi kwa mazoea, lakini kiukweli tatizo bado lipo kwani
wanaoambiwa kama vile hayawahusu.
Ukiingia kwenye
taasisi za umma hivi sasa utoaji wa huduma umezorota sana, kwani baada ya
mfanyakazi kumhudumia mwananchi aliyefika kwenye taasisi kutaka huduma,
mfanyakazi anachati kwa mambo ya kipuuzi kwenye mitandao ya kijamii.
Wapo baadhi ya
watumishi wa umma kutwa wapo ‘online’, kupitia simu zao za mikononi wakipokea
habari za kipuuzi na za kijinga ambazo hazina na wala hazihusiani na uwajibikaji
wa mtumishi, hata muda wa kutoa huduma kazini hana.
Hivi kweli kwa
tabia hizo za kukaa ‘online’ kila wakati, dharura zisizo na umuhimu
zisizokwisha zitasaidia kupatikana maendeleo na ufanisiki kwneye majukumu ya
mfanyakazi.
Tumekuwa wapesi
wa kupiga keleke kudai nyongeza za mishahara na maslahi mengine sio vibaya
kufanya hivyo, lakini je tumejitathimini kwenye utendaji na uwajibikaji wetu?
Kama hatujaonesha
ufanyakazi mzuri wenye tija na faida kubwa huyo mwenye mamlaka ya kupandisha
mishahara kweli atahamasika kufanya hivyo? Leo ni siku muafaka kujitathimini na
kujihakiki kwa kila mmoja wetu.
Tukumbuke ule
msemo mashuhuri, haki na wajibu ni watoto pacha, tuwajibike kwa mafanikio,
hakutakuwa na kipingamizi cha kupata haki.
Post a Comment