Header Ads

'Ongezeni Mashirikiano kufanikisha shughuli za Serikali kwa Wananchi'

VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi CCM, Jimbo la Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wametakiwa kuongeza mashirikiano katika usimamiaji wa shughuli za serikali ili kuhakikisha Ilani chama hicho inatekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Shamata Shaame Hamis katika kikao cha Viongozi kutoka katika Wadi za Jimbo, cha kutathimini utendaji kazi wa viongozi hao katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Akizungumza katika kikao hicho, mwakilishi huyo alisema ili Serikali iweze kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ni lazima viongongozi kuwa msitari wa mbele kwa kuendelea kuwajibika katika nafasi zao.

“Tumepewa dhamana na chama kuhakikisha tunaisaidia Serikali iweze kutekeleza kikamilifu yale yaliyoahidiwa katika ilani ya uchaguzi, hivyo nikuombeni muendelee kuwajibika kila mtu kwa nafasi yake,” alisema Shamata.

Aidha alisema licha ya kuwepo kwa utekelezaji wa miradi kwa kiwango kikubwa katika jimbo la Micheweni, lakini bado mashirikiano yanahitajika zaidi.

“katika jimbo letu la Micheweni tunashukuru tumefanikiwa kutekeleza Miradi mbalimbali, ikiwemo uchimbaji wa Visima vya Maji pamoja na ujenzi wa Ukumbi wa Mitihani Skuli ya Kiuyu Maziwang’ombe, ambapo haya yote yamefanikiwa kutokana na mashirikiano yenu,” Shamata alisema.

Akichangia mmoja wa viongozi waliohudhulia kikao hicho, Ali Khamis Mbwana, aliahidi kuendeleza mashirikiano katika chama kijimbo, pamoja na kuongeza uwajibikaji ili kuhakikisha CCM inaendelea kuaminika kwa Wananchi wake.

“Sisi kama viongozi wa chama kijimbo tutaendelea kutoa mashirikiano yetu ili kusudi kuona kwamba CCM inaendelea kushinda katika chaguzi zote,”alisema.

Mkutano huo wa Mwakilishi na Viongozi mbalimbali wa Jimbo la Micheweni ni Mwendelezo wa juhudi za Mwakilishi huyo za kuwakumbusha viongozi wajibu  katika nafasi zao ikiwa ni pamoja na kusisitiza uwajibikaji katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2015.


No comments