'Sina Msamaha kwa Fisadi wa Pesa za Umma'- Dk. Shein
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema uchumi wa Zanzibar umeendelea
kuimarika kutokana na uongozi thabiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
kusisitiza kuwa hatokuwa na msamaha kwa yeyote atakaebainika kufanya ubadhirifu
wa fedha za umma.
Dk. Shein aliyasema hayo
katika ukumbi wa Jamhuri Wete wakati alipokuwa akizungumza na mabalozi wa
wilaya ya Wete, mkoa wa kaskazini Pemba.
Alifahamisha kuwa uchumi wa
Zanzibar umekuwa ukiimarika kwa kiasi kikubwa na kutumia fursa hiyo kuendelea
kusisitiza kauli yake aliyoitoa katika maadhimisho ya kilele cha Mei Mosi mwaka
huu, kuwa wale wote wanaodiriki kufanya ubadhirifu wa fedha za umma
watashughulikiwa.
Alieleza jinsi Zanzibar
ilivyokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha na uchumi hatua iliyompelekea kuongeza
mishahara mara nne katika uongozi wake sambamba na kuimarikaka kwa sekta za
maendeleo.
Aliendelea kusisitiza kauli
yake kuwa ataendelea kuiongoza Zanzibar kwa uadilifu mkubwa na kusisitiza kuwa
viongozi wote walioteuliwa wanatekeleza ilani ya CCM.
Aliwaeleza viongozi hao kuwa
ujenzi wa Chuo cha Amali cha Daya-Mtambwe utaanza hivi karibuni na ujenzi wa
barabara ya Finya-Kicha itakayojengwa kwa kiwango cha lami sambamba na
kuzitafutia ufumbuzi changamoto nyengine walizoziorodhesha.
Akiwaeleza wajibu wao kwa
mujibu wa katiba ya CCM, aliwaeleza viongozi hao wajijue kuwa wao ni wenezi na
wahamasishaji wakuu wa CCM pamoja na kuwa na wajibu wa kuwaeleza wanachama
katika maamuzi yote ya CCM na kufikisha mapendekezo ya wanachama katika vikao
vya juu.
Alisema wanaCCM wote wakiwemo
viongozi hao wana kazi kubwa ya kufanya katika kusaidia ushindi wa CCM na kila
mmoja kwa ngazi yake kwa namna yake na kuwa na wajibu wa kufanya yeye mwenyewe
kwa uwezo wake kusaidia ushindi huo.
Aidha, alisisitiza kuwa
ushindi kwa CCM ni suala la lazima kutokana na maelekezo ya katiba ya chama
hicho na hakuna mbadala wa ushindi kwa kufuata taratibu na namna zote za
kidemokrasi kwa lengo la kuyalinda Mapinduzi ya Januari 12,1964 pamoja na Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Post a Comment