Header Ads

ZAECA Kas Pemba Kuwatumia Wasanii Kutoa Elimu kwa Wananchi

MAMLAKA ya kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) Mkoa wa Kaskazini Pemba, imebuni mbinu mpya za utoaji wa elimu ambapo imeanza kuwatumia wasanii wa maigizo kufikisha ujumbe wa jamii.

Akizungumza na REDIO JAMII MICHEWENI, msanii  wa maigizo Khatib Omar Khatib (Kitatange) amesema sanaa ni moja ya njia bora za kutumia katika kufikisha ujumbe kwa jamii na hupokewa kwa wakati muwafaka.

Amesema katika kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Mamlaka hiyo, atahakikisha anashiriki kikamilifu katika kuielimisha jamii ili ijiepushe na matendo ya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Kitatange ameahidi kutumia ujuzi na taaluma yake kufikisha ujumbe kwa wananchi ili kuwafanya kuzifahamu athari za matendo ya rushwa ambayo yanasababisha jamii kununua haki.

“Sanaa ni njia bora katika kupeleka ujumbe kwa jamii, hivyo naahidi kutumia ujuzi wangu kufikisha ujumbe wa rushwa kwa wananchi” alieleza.

Naye Maariam Saalim Juma amesema bado itachukua muda kuweza kufanaaikisha vita dhidi ya rushwa kwa kuwa wapo wananchi wanaochangia kutoa rushwa bila ya kudaiwa.

Amesema ili mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi  yaweza kufanikiwa ni budi  jamii  kuhakikisha inashiriki kupiga vita matendo hayo.

Mdhamini wa Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi Mkoa huo Abubakar Mohammed Lunda amesema mamlaka imekuwa ikikosa taarifa za matendo hayo kutokana na jamii kutokuwa na uwelewa wa kuyaripoti matukio hayo.

Amesema kwamba baada ya kuyabaini hayo , Mamlaka imeamua kutembelea maeneo ya vijijini kutoa elimu ambapo moja wa washiriki wa kampeni hiyo ni wasanii wa maagizo.

“Tumebaini kwamba taarifa nyingi zinazohusu matendo ya rushwa na uhujumu wa uchumi zinakosekana , hivyo kwa kutambua hilo Mamlaka imeamua kufika hadi vijijini kwa ajili ya kutoaa elimu kwa wananchi” aalifahamisha.

Aidha Abubakar amesema kutokana na wajibu wa kikatiba, ni vyema viongozi wa dini kuipa ushirikiano Mamlaka katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuchukua hatua za makusudi kukemea matendo hayo.

Kwa mujibu  wa Ibara ya 10(b) ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inaeleza kuwa moja ya jukumu la Serikali ni kupambana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

No comments