Header Ads

'Malezi bora kwa watoto ni pamoja na mashirikiano ya malezi


WAZAZI na walezi katika shehia ya kiuyu mbuyuni wilaya ya micheweni mkoa wa kaskazini pemba wametakiwa kushirikiana kwa pamoja katika suala la malezi ili kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki ya msingi ya elimu.

Ushauri huo umetolewa na afisa miradi wa SOS Pemba Gharib Abdallah Hamad katika ukumbi wa mitihani wa skuli ya kiuyu mbuyuni wakati alipokuwa akizungumza na wazazi hao.

Amesema lengo la mkutano huo ni kutaka kujua changamoto zinazowakabili watoto wa kike katika sekta ya elimu na kuweza kuangalia namna ya kuzitatua.

Akichangia katika mkutano huo Makame Kombo Hamad ambae ni katibu wa kamati inayosimamia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ndani ya shehia hiyo amesema umasikini uliokithiri pamoja na uelewa mdogo wa wazazi na jamii juu ya umuhimu wa elimu ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake Ali Masoud Kombo ambae ni meneja wa kituo cha redio jamii micheweni amesema kituo chake kimekuwa kikitoa elimu mashuleni kuhusu suala la elimu kwa mtoto wa kike kupitia miradi mbali mbali inayofika kituoni hapo.

Amesema tayari skuli nne za wilaya hiyo tayari zimefaidika na mafunzo hayo ambapo skuli hizo ni Micheweni Sekondari, Wingwi Sekondari, Shumba vyamboni pamoja na Skuli ya Chwaka Tumbe.

No comments