Mke apewa kipigo kisa kukutwa akivunja maadili ya ndoa MICHEWENI
Picha na Maktaba |
JESHI
la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, limesema baada ya kumaliza kumuhoji, kaimu Sheha wa Shehia ya Chimba Wilaya ya Micheweni, Hamad Aayoub Khamis, kwa tuhuma
za kumpiga mke wake kwa wivu wa mpenzi, litampandisha kizimbani pindi
upelelezi ukikamilika.
Kamanda
wa Polisi mkoa huo, Hassan Nassir Ali, amesema ni kweli Kaimu sheha huyo, juzi
alihojiwa kutokana na kitendo cha kumpiga mke wake Juni 3, baada ya kudaiwa
kumkuta akiwa na mwanamme.
Akizungumza
na vyombo vya habari, alisema baada ya kumuhoji sasa kilichopo kwa Jeshi hilo,
ni kuendelea na upelelezi wa kina wa tukio hilo, na pindi ukihusisha na tukio,
atapandishwa mahakamani.
Kamanda
Nassir, alisema baada ya kupokea malalamiko ya mwanamke mmoja miaka 38 kupigwa
na mume wake, ndipo Jeshi hilo lilimpomtafuta na kumpata, na kisha kumuhoji,
kwa kupata maelezio zaidi.
‘Ni
kweli yupo kaimu sheha wa shehia ya Chimba, alimpiga mke wake na sisi Jeshi la
Polisi tumeshamuhoji, na kilichobakia ni upelelezi, kwa lengo la kumfikisha
mahakamani hapo baadae,”alieleza.
Hata
hivyo, Kamanda Nassir ameendelea kutoa wito kwa wale wanaokosa, kuacha
kujichukulia sheria mikononi, na badala yake wavitumie vyombo vya sheria
kulalamika.
Akizungumza
na mwandishi wa habari kwa njia ya simu, Kaimu sheha huyo wa shehia ya Chimba,
alikiri kumfumania mke wake nje ya
nyumba yake, ingawa hakuthubutu kumpiga kama inavyodaiwa.
Alisema,
baada ya kumfuma akiwa katika mazingira hatarishi, alichokifanya ni kumpapatuana,
na yule mwanamme wa nje, ambapo hapo mke
wake, alianguka chini na kisha kukimbilia hospitali na Polisi, akidai kuwa
amepigwa.
“Aliniaga
anakwenda kwa shoga yake, muda mfupi tu baada ya kumaliza kufutari hapo juzi,
sasa mimi nikamfuatilia na kiasi ya masafa ya viwanja vitatu vya mpira (mita
300), nikamkuta kwenye nyumba na mwanamme wamekumbatiana hapo nikampapatua,”alisimulia.
Kaimu
sheha huyo alieleza kuwa, yeye hajampiga na wala hajamucha mwanamke huyo,
ingawa kwa sasa ameshachukuliwa na familia yake na hayupo nyumbani kwake.
“Mimi
sijampiga, nilichofanya nilimpapatua mke wangu na yule jamaa, lakini pamepikwa
mambo kuwa, nimempiga na wajomba zake, wamemchukua ingawa
sijamuacha,’’ alifafanua.
Kuhusu
kuhojiwa Polisi, Kaimu sheha huyo alithibitisha kuhojiwa na kulala kituo cha
Polisi kwa siku moja, ambapo alisema ataitwa tena kama akitahitajika juu ya
tuhuma hizo.
Mwanamke
huyo, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alikana kufumaniwa na mume
wake, ingawa alikiri kupokea kichapo na sababu kubwa, akisema ni chuki ya mume
wake.
“Unajua
huyu mume wangu, anachuki zake muda mrefu sasa kanipiga kaniumiza, eti kisha
anadai kunifumania, uongo mtupu, mwezi huu mimi muislamu nifanye
hivyo,”alihoji mwanamke huyo.
Alieleza
kuwa, kama kweli amefanya jambo hilo ovu na kubwa, wala wajomba zake
wasingekuwa pamoja nae, na kumkimbiza kwa mume wake, lakini kwa vile amenipiga
kwa chuki na hamaki zake, ndio maana amehifadhiwa kwao.
Mkuu
wa wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib, ambae anadawi kumsaidia kumtoa sheha
huyo kituo cha Polisi, alikana na kusema hata siku ya tukio hakuwepo mazingira
ya kazi.
“Mimi
sina taarifa mwandishi, maana hata siku ya tukio nilikuwa nje ya eneo la kazi,
sasa sina taarifa na wala silijui kwa kweli,”alijibu Mkuu huyo wa Wilaya.
Kaimu
sheha huyo, ameshazaa watoto watano na mke wake huyo, ambapo kwa sasa mwanamke
huyo yuko kwa ndugu na jamaa zake na kuwaacha watoto wake wote.
Hili
ni tukio la kwanza la aina yake kutokea katika kipindi cha miongo mitatu sasa,
cha mume kumkuta mke wake akiwa katika mazingira ya kuvuuka maadili.
Post a Comment