Header Ads

Wananchi Shehia ya Maziwang'ombe waungana kutokomeza utoro mashuleni


WAZAZI, Kamati za Sikuli na Walimu katika Shehia ya Maziwang’ombe, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa pamoja wamependekeza kuwepo kwa mikakati itakayowabana wazazi wanaoshindwa kuwahamasisha watoto wao kwenda skuli.

Maamuzi hayo yamekuja katika kikao cha Wazazi, kamati za Skuli pamoja na walimu cha kutathimini maendeleo ya upatikanaji wa haki ya elimu kwa watoto katika Sikuli ya Msingi Maziwang’ombe kwa kuandaliwa na Shirika la SOS Children’s Village Zanzibar.
Wshiriki wakifuatilia mada inayowasilishwa na Afisa Miradi kutoka Shirika hilo, Gharib Abdallah Hamad
Akichangia katika kikao hicho Time Abdallah Hassan, amesema kuwa watoto kuendelea kukimbia skuli ni kutokana na kutokuwepo kwa hatua zozote ambazo wazazi wanachukuliwa kwa kushindwa kuwahimiza watoto wao kwenda skuli.

“Ifike pahala sisi wenyewe tujiwekee mikakati ambayo itawabana wazazi ambao watoto wao hawaendi skuli, naamini mzazi akisikia kuna Fulani kufungwa kutokana na mwanae kuacha kwenda skuli, lazima atamhimiza mtoto wake aende skuli ili nayeye yasimpate,” alisema Bi Time.

Awali akichangia, Sheikh Omar Hussein Said amesema kuwa wazazi wengi wa sasa wanakosa uhamasishaji juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao ikilinganishwa na hapo zamani.
Wshiriki wakifuatilia mada inayowasilishwa na Afisa Miradi kutoka Shirika hilo, Gharib Abdallah Hamad
“Leo hii mtoto anaacha kwenda skuli na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa mzazi wala mtoto mwenyewe, naamini kama Serikali itaamua kuanza kuwachukulia hatua wazazi kwa kuwafikisha mahakamani na pengine kuwafunga kabisa tatizo hili litamalizika na sidhani kama kutakuwa na mzazi tena ataacha kumhimiza mtoto wake kwenda skuli wakati anajua anaweza kufungwa,” alisema Sheikh huyo.

Mwalimu mkuu wa Skuli hiyo, Hemed Shaame Shoka, amesema walimu kwa kiasi kukubwa wanakosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wazazi na kupelekea watoto kukosa haki yao ya elimu ambayo husababishwa na utoro.

“Ni lazima tukubali kwamba wazazi nao ni chanzo kikubwa cha watoto kuikosa haki hii ya elimu kwani wazazi wengi tunapowaita katika vikao vyetu vya wazazi, wengi wao hawahudhulii,” alisema Mwalimu Hemed.
Licha ya kutajwa mambo mbalimbali ambayo hupelekea watoto kuwa watoro mashuleni, lakini pia suala la uhaba wa walimu limetajwa kuhusika kutokana na walimu kuelemewa na wingi wa wanafunzi madarasani.
Mmoja wa washiriki akichangia mada
Bi Awena Hamad Kombo mwananchi katika shehia hiyo amesema walimu wanashindwa kufuatilia maendeleo ya wanafunzi wao kutokana idadi ya wanafunzi waliopo mashuleni haiendani na idadi ya walimu.

“Tusiwalaumu watoto tu kwamba hawapendi kusoma lakini hata hali iliyopo mashuleni pia inachangia kuwakatisha tamaa watoto kwenda skuli kwani unakuta darasa moja lina wanafunzi 200 na linafundishwa na mwalimu mmoja, hivi unategemea hawa watoto wote watamsikiliza mwalimu kweli kwa pamoja?,” aliuliza.
Afisa wa Elimu Wilaya ya Micheweni, Tarehe Hamis Hamad, akizungumza katika kikao hicho.
Afisa wa Elimu Wilaya ya Micheweni, Tarehe Hamis Hamad amepongeza maamuzi ya washiriki hao na kuahidi kushirikiana nao kwani yanalengo la kuimarisha elimu katika Wilaya hiyo.
Afisa Miradi kutoka Shirika la SOS Pemba, Gharib Abdallah Hamad, akiwasilisha mada kwa washiriki.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Afisa Miradi kutoka Shirika hilo, Gharib Abdallah Hamad amewataka wazazi, kamati ya skuli, walimu pamoja na Serikali ya Wilaya kukaa pamoja na kutafta njia bora ya kuweza kufanikisha kwa mikakati hiyo.

Miongoni mwa mikakati waliyojiwekea washiriki hao ni pamoja na kuunda kamati maalum ya Shehia itakayo simamia maendeleo ya elimu kwa watoto ikiwa ni pamoja na, kuweka sheria za kuwawajibisha waajiri wa watoto, kuwawajibisha wazazi wanaowatorosha watoto wao kwa kuwafikisha kituo cha polisi na kupigwa faini.

No comments